Lindi. Baadhi ya viongozi wa dini, vyama vya siasa na watu wenye ulemavu mkoani hapa, wametaka kuimarishwa kwa amani na haki wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumza leo Ijumaa Septemba 27, 2024 wakati wa kutoa ratiba ya ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Mwenyekiti wa kamati ya viongozi wa dini mkoani wa Lindi, Mchungaji Canon Marcos amewataka wananchi kushiriki uchaguzi huo bila vurugu.
“Kuna maisha nje ya uchaguzi, hivyo niwaombe wananchi wa Manispaa ya Lindi kuhakikisha tunafanya uchaguzi kwa amani na utulivu ili kuweza kudumisha amani yetu, sisi sote ni Watanzania hatuna budi kudumisha amani yetu,” amesema Marcos.
Katika hatua nyingine, Katibu wa Jimbo la Lindi mjini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Martine Kanangu amemtaka msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi, kufuata utaratibu unaotakiwa wakati wa kupiga kura ili kuepusha vurugu.
“Chaguzi nyingi za serikali za mitaa tunashirikishwa vizuri, lakini inapofikia hatua ya kwenda kupiga kura mambo yote yanabadilika, tunaomba msimame kwenye misingi ya haki kwa ajili ya mstakabali wa Taifa letu,” amesema Kanangu.
Aidha, watu wenye mahitaji maalumu akiwemo mwenye ulemavu wa miguu Martha Juma, wamesema kuwa wataweka kipaumbele kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali, licha ya wao wenyewe kujirudisha nyuma kuona kwamba hawatachaguliwa.
“Sisi watu wenye mahitaji maalumu tumekuwa tukijirudisha nyuma kuona kwamba hatutachaguliwa. Tunatakiwa kujipa moyo sisi wenyewe ili kuweza kugombea nafasi mbalimbali,” amesema Juma.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi, Juma Mnwele amewataka wananchi wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali na kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kupiga kura kuanzia Oktoba 11 hadi 20, 2024.