Iringa. Jeshi la Polisi nchini limewaonya abiria wanaochochea madereva wa vyombo vya usafiri kuwa na mwendo usio salama, kwani huo ndio mwanzo wa kutokea ajali.
Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 28, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Usalama Barabarani nchini, Michael Deleli wakati akizungumza katika maadhimisho ya miaka 10 ya Baraza la Usalama Barabarani (RSA).
Amesema jeshi hilo linajitahidi kudhibiti ajali lakini abiria ndio wamegeuka kuwa wachochezi na kusababisha ajali wakilazimisha madereva wa vyombo vya usafiri kuendesha kwa mwendo usio stahili.
“Tunajitahidi kudhibiti hili lakini abiria ndio wachochezi wa ajali, ukienda kwenye vituo vya mabasi magari yanayokimbia sana tiketi zinaisha mapema hivyo abiria ni wapenzi wa mwendo kasi,” amesema ACP Michael Deleli.
Amesema hali hiyo ni ishara kuwa Watanzania wengi bado hawana elimu ya usalama barabarani.
Amesema katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2024 Jeshi la Polisi limetoa elimu ya usalama barabarani kwa Watanzania wapatao milioni 16.
Deleli ameongeza kwa kusema kwa sasa inaumiza sana kuona Watanzania wengi wanatumia muda wao mwingi kuuguza waathirika wa ajali za barabarani.
Hata hivyo, ACP Deleli amesema asilimia 75 ya ajali zinatokana na makosa ya kibinadamu, huku asilimia 25 ya ajali zikitokana na ubovu wa magari pamoja na ubovu wa miundombinu.
Pamoja na mambo mengine amesema kundi ambalo linaangaliwa kwa macho makubwa ni pikipiki ambazo zinachangia ajali nyingi kutokana na wingi wake.
“Kwa sasa tuna pikipiki zipatazo milioni mbili zilizosajiliwa na magari milioni moja yaliyosajiliwa, hivyo kundi ambalo tunaliangalia kwa macho makubwa ni pikipiki ambayo inaweza kuingia na kusabisha ajali hadi sebuleni,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa RSA, Augustus Fungo, amesema changamoto wanazo kutana nazo ni mitazamo ya watu ambao wanaona kama taasisi hiyo inaingilia kazi za polisi katika kutoa elimu ya usalama barabarani.
Amesema wao hawakagui magari wala kuyakamata bali wao ni mabalozi wa kutoa elimu ya usalama barabarani na kuripoti matukio ya ajali.
“Sisi hatukagui magari wala kuyakamata bali tunatoa elimu na kuripoti matukio yanayotokea barabarani,” amesema Fungo.
Fungo ameshauri Serikali kufanya mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani akisema kwa sasa imepitwa na wakati.