Ajibu: Wala hatuna presha na Simba

KIUNGO mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Ibrahim Ajibu amesema mechi dhidi ya Simba itakayopigwa kesho Jumapili jijini Dodoma, haina utofauti na mechi zingine ambazo wamecheza Ligi Kuu.

Dodoma itaialika Simba kwenye  Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ikiwa ni muendelezo wa Ligi Kuu, huku ikiwa na rekodi mbaya ya kuwatowahi kushinda wala kutoka sare mbele ya Mnyama, lakini Ajibu alisema msimu timu hiyo inakuja kivingine kuwakabili wapinzani wao.

Ajibu alisema kama wachezaji hawana hofu juu ya Simba kwani ni timu kama nyingine zinazoshiriki Ligi lakini wakiingia kwenye mchezo huo kwa kuuheshimu ubora wa wapinzani wao.

“Utofauti labda mashabiki kwa sababu unapocheza na timu kama Simba inakuwa na wingi wa mashabiki hivyo tunaweza kuhimili presha yao,” alisema Ajibu

Kuhusu mwenendo wa timu hiyo alisema; “Tumecheza mechi tano na tumekusanya pointi sita sio mwanzo mbaya kwetu kwa sababu kuna timu zimepoteza zote hivyo kwetu ni kuendelea kupambana tu.”

Hadi sasa tayari Dodoma imecheza mechi tano ikishinda mechi moja dhidi ya Namungo 1-0, sare tatu Pamba Jiji 0-0, Fountain Gate 2-2 na 0-0 Prisons huku ikipoteza dhidi ya Mashujaa bao 1-0 ugenini.

Related Posts