Geita. Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Geita imeamuru mshtakiwa John Alex aliyekuwa akishtakiwa kwa kosa la kumuua mtoto Revina Joseph (2) kutunzwa katika Taasisi ya wagonjwa wa akili Isanga kama mhalifu mgonjwa wa akili.
Katika kesi hiyo namba 59/2022 iliyokuja kwa ajili ya usikilizwaji Jaji wa Mahakama hiyo, Athuman Matuma ametoa uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili pamoja na taarifa ya uchunguzi wa afya ya akili ya mshtakiwa.
Akitoa maamuzi hayo Jaji Matuma, amesema kwa kuzingatia hati ya mashtaka aliyoshtakiwa nayo na hoja zilizotolewa mahakamani hapo na kuzingatia taarifa ya kifo pamoja na taarifa ya uchunguzi wa akili ya mshtakiwa, inadhihirisha kuwa ni kweli alitenda kosa hilo la mauaji lakini hakuwa na akili timamu.
“Mahakama inatoa amri maalum ya kwamba mshtakiwa ni mkosaji lakini mgonjwa wa akili chini ya kifungu cha 2019(2) cha sheria ya mweneydo wa jinai sura ya 20 marejeo 2019, naamuru atunzwe kwenye taasisi ya magoinjwa ya akili Isanga atunzwe kama mhalifu mgonjwa wa akili “
Jaji Matuma ameongeza kuwa mshtakiwa huyo atunzwe kwa mujibu wa kifungu cha 2019(3a)cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai hivyo ahudumiwe na kushughulikiwa kwa mujibu wa kifungu cha 2019 (4,5 na 6)cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Mshtakiwa huyo John Alex Mkazi wa Buziku Wilayani Chato mkoani Geita alishtakiwa kwa kosa la mauji kinyume na kifungu cha 196/197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 ya mwaka 2019.
Ilidaiwa Mahakamani hapo kuwa Juni 20,2021 mshtakiwa alimpiga kichwani na kipande cha mti Revina na kumsababishia majeraha yaliyosababiisha kifo chake.
Wakati wa usikilizaji wa hoja za awali wakili wa upnde wa utetezi, Vianey Mbuya aliibua hoja ya kuwa mteja wake ana matatizo ya akili na mahakama ikaamuru apelekwe kwenye taasisi ya uchunguzi wa akili kwa ajili ya uchunguzi wa afya ya akili.
Shauri hilo upande wa Jamhuri uliongozwa na mawakili Luciana Shaban akisaidiana na Kabula Benjamin huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Vianey Mbuya.