BILIONI 15 KUSAMBAZA UMEME KATIKA VITONGOJI 105 MKOA WA ARUSHA 

 

MKUU wa Mkoa wa Arusha Mhe.Paul Makonda,akizungumza na wananchi wakati mara baada ya kumkabidhi Mkandarasi tenda atakayetekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji vya mkoa wa Arusha

SEHEMU ya wananchi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.Paul Makonda (hayupo pichani) ,akizungumza  mara baada ya kumkabidhi Mkandarasi tenda atakayetekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji vya mkoa wa Arusha

Na.Mwandishi Wetu

MKUU wa Mkoa wa Arusha Mhe.Paul Makonda  ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi nzuri ya kutekeleza miradi ya kusambaza  umeme vijijini.

Mhe.Makonda ameyasema hayo jijini Arusha wakati wa kumtambulisha na kumkabidhi Mkandarasi atakayetekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji vya mkoa wa Arusha

Amesema kuwa miradi ya kusambaza umeme vijijini imewezesha wananchi kuunganishiwa umeme kwa gaharama nafuu na imeondoa dhana kuwa umeme ni wa matajiri.

Aidha amemtaka Mkandarasi aliyetambulishwa kutekeleza  mradi huo kwa weledi na kwa kuzingatia muda wa mkataba aliopewa.

“Tunamtaka Mkandarasi kutekeleza mradi huo kwa uaminifu na hatutasita kuchukulia hatua pindi atakavyoshindwa kutekeleza kwa wakati na pia tunamtaka Mkandarasi kutumia vijana wetu waliopo katika mkoa wa Arusha  kutekeleza mradi huo.

Naye Mkurugenzi wa umeme Vijijini REA, Mhandisi Jones Olotu,amesema kuwa  jumla ya vitongoji   1,039  vitapatiwa umeme  kupitia mradi huu.

“Vitongoji 105 kati ya 1,039 vilivyobaki vitapata huduma ya umeme kupitia mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji vyote nchini (HEP Densification project).”

Mhandisi Olotu alimtambulisha Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni kampuni ya CEYLEX ENGINEERING (Pvt) LTD  na gharama ya mradi huo ni takribani shilingi bilioni 15 na utanufaisha wateja wapatao  3,465.

Related Posts