Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka wananchi kuimarisha amani akisema haijengwi kwa kumwaga damu bali kwa kuelewana.
Amesema hayo leo Septemba 28, 2024 akiwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya amani Mkoa wa Dar es Salaam yalifanyika kwenye viwanja vya Mwembeyanga wilayani Temeke.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni ‘Dumisha amani shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.’
Amesema endapo yakitokea machafuko idadi kubwa ya watu watapata tabu kulingana na aina ya maisha wanayoishi.
“Tunapozungumzia amani ni msingi wa maendeleo kwa sababu maendeleo bila ya amani hayawezi kuwepo,” amesema.
Chalamila amewataka Watanzania wasidanganywe kushiriki maandamano akisema Serikali imejipanga kudhibiti wanaopanga kuvuruga amani nchini.
“Dar es Salaam tukipachafua pasitawalike kwa muda wa wiki moja tu nina uhakika maiti zitakazookotwa zitakuwa nyingi kwa sababu wakazi wa Dar es Salaam, hawana hifadhi ya chakula,” amesema.
Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Tob Nguvila amewataka wananchi kutambua umuhimu wa amani na hasa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, 2024.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo akiwakilisha wakuu wa wilaya mkoani hapa, amesema wapo tayari kuimarisha Amani.
“Nikiwakilisha wakuu wa wilaya zote za Dar es Salaam, tupo tayari kuimarisha amani kwa sababu huu ndiyo mkoa wenye idadi kubwa ya watu, lakini pia ndio mkoa wenye shughuli nyingi za kiuchumi,” amesema.
Amesema wapo tayari kupokea na kufanyia kazi maagizo watakayopatiwa na Serikali.