Mwanza. Bismarck Rock au Jiwe la Bismarck ni jiwe maarufu siyo tu kwa wakazi wa Jiji la Mwanza, bali pia wageni kutoka ndani na nje ya nchi wanaotembelea jiji hilo.
Jiwe hilo lipo juu ya mawe yaliyojipanga kwa upekee ndani ya maji ya Ziwa Victoria, kana kwamba yamepangwa na kundi la wahandisi wabobevu tena kwa kutumia zana na vifaa vya kisasa.
Mawe haya yanapatikana kwenye ufukwe wa ziwa hilo eneo la Kamanga, na ni moja vivutio vya utalii vinavyopatikana ndani ya Jiji la Mwanza lililojaaliwa vivutio vingi ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Saanane ambayo ni hifadhi pekee nchini inayopatikana katikati ya jiji.
Kutokana na upekee na umaarufu wa mwamba huo, siyo tu wageni wanaofika Mwanza hutembelea eneo hilo, bali hata wenyeji hutumia muda wao wa mapumziko kuvinjari na kufaidi mazingira, hewa safi na upepo mwanana kutoka ziwani.
Wafanyabiashara hasa wa boti ndogo zinazotumika kutembeza wageni katika maji ya karibu na ufukweni, wajasiriamali wa bidhaa mbalimbali na wapigapicha za mnato na jongefu, ni kati ya makundi ya kijamii yanayonufaika na uwepo wa mawe hayo.
Baadhi ya wenyeji wa Mkoa wa Mwanza wanadai kabla ya jina la sasa la Bismarck jiwe hilo lilijulikana kwa jina la ‘Jiwe la Mwanamalundi’ (Ng’wanamalundi), likiwakilisha jina la jemedari, mcheza ngoma maarufu na mganga wa jadi aliyejaa maajabu kutoka jamii ya Wasukuma aliyeonyesha uhodari katika mapambano dhidi ya ukoloni enzi hizo..
Jina Mwanamalundi lilitokana na miguu yake kuwa myembamba na mirefu.
Wanasema jiwe hilo lilipewa jina la Mwanamalundi kwa kuwa ni miongoni mwa maeneo aliyotembelea, kucheza ngoma na kuonesha maajabu yake ikiwemo kuchomeka mikuki sita juu ya mawe hayo ambayo inadaiwa ipo mpaka leo hii.
Pamoja na mikuki hiyo iliyopo katika mawe yanayolibeba jiwe la Bismack, kuna alama zingine zinazodaiwa kuachwa na Mwanamalundi ikiwemo nyayo za miguu yake, alama ya makalio na sehemu inayosemekana ilikuwa kitanda chake.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Machifu nchini ambaye pia ni Chifu wa Mkoa wa Mwanza, Aron Mkomangwa anasema kabla ya ukoloni, jiwe hilo liliitwa jiwe la Kapigipondo ikiwa na maana ya jiwe lililoko eneo la faragha.
“Jiwe lilikuwepo karne na karne na lilikuwa linaitwa jiwe la Kapigipondo, yaani jiwe lililoko eneo la faragha,”anasema Chifu Mkomangwa.
Kuhusu nondo zilizopo kwenye mawe hayo zinazodaiwa kuwa ni mikuki ya Mwanamalundi, anasema:
“Nondo zilizoko kwenye jiwe hilo ziliwekwa na Wajerumani wakitafiti na kupanda hapo juu, siyo Ng’wanamalundi ni uongo wa hali ya juu….Ng’wanamalundi hakuishi Mwanza bali aliletwa kama mfungwa,”
Kwa mujibu wa Mtembeza watalii katika mwamba huo, Silvester Benson anasema baada ya ujio wa Wakoloni wa Ujerumani kuanzia miaka ya 1886, aliyekuwa Kansela wa Ujerumani wakati huo, Otto Van Bismarck alijaribu mara kadhaa kuharibu jiwe hilo bila mafanikio.
Anasema Kansela huyo aliyekuwa kiongozi wa kisiasa na mwanafalsafa wa Kijerumani ambaye pia alijulikana kama mchora mipango wa Ujerumani kutokana na mbinu na juhudi zake za kuunganisha majimbo mbalimbali ya Kijerumani kuwa taifa moja, alipeleka watumwa kuangusha jiwe hilo bila mafanikio.
Ofisa habari wa Jiji la Mwanza, Martin Sawema anasema kutokana na uimara na kutoharibika wala kuanguka kwa jiwe hilo, Kansela huyo aliamua kulipa jiwe hilo jina lake akiamini ni mwamba imara kama yeye, na ndipo jina la Bismarck Rock lilipozaliwa.
Hata baada ya kuondoka Tanganyika, wafuasi wake waliamua kujenga sanamu yake pembeni mwa jiwe hilo ambalo hata hivyo baada ya Wajerumani kushindwa kwenye vita ya kwanza ya dunia na Tanganyika kuwa chini ya koloni la Uingereza, sanamu hiyo ilivunjwa.
“Inadaiwa Mwingereza alivyotawala alilivunja sanamu la Bismarck, masalia yake yapo ziwani hadi leo,”anasema Benson.
Maajabu ya jiwe la Kapigipondo
Miongoni mwa maajabu ya jiwe hilo yanayovutia watembeleaji, ni namna jiwe hilo lilivyoungana kwa sehemu ndogo bila kuanguka.
Hata mbabe, Bismarck inaelezwa kuwa alitokwa na kamasi alipotaka kulivunja, akaambulia patupu!
Kama haitoshi mwonekano wa namna mawe yalivyojipanga eneo hilo, umekuwa maajabu yanayowavutia watu wengi.
Wanavyosema watalii wa ndani
Mtalii wa ndani kutoka mkoani Arusha, Vumilia Timotheo anasema alikuwa analiona jiwe hilo kwenye runinga, mitandaoni na kwenye majarida hivyo alipofika mkoani Mwanza miongoni mwa vitu alivyolenga kufanya ni kutembelea jiwe hilo.
“Nimetembelea na kujionea jiwe hili, nimevutiwa pia na kupanda boti kwa sababu sijawahi kupanda nakuona mandhari nzuri ya ziwa…lakini pia nimejifunza maajabu ya Mwanamalundi, alikuwa ni mtu mwenye nguvu za kipekee, nimeona pia alipo kanyaga na kuacha unyayo wake kwenye jiwe,”anasema Timotheo.