Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini, ametoa maelezo muhimu kwa umma kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, utakaofanyika tarehe 27/11/2024, kwa lengo la kuhakikisha kuwa taratibu zote zinafuatwa, na Wapiga Kura pamoja na wagombea wanapata taarifa zote zinazohitajika kwa wakati.
Maelekezo haya yanafafanua hatua zitakazoongoza mchakato wa uchaguzi, kuanzia uandikishaji wa Wapiga Kura, uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea, uteuzi wa Wagombea na tarehe ya siku ya uchaguzi. Maelekezo hayo ni mwongozo wa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na usawa na kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizowekwa.
Mhandisi Hamsini amesema, Halmashauri ya Jiji la Tanga yenye jimbo moja la uchaguzi, ina Kata 27 na mitaa 181, na kwamba ni jukumu kila mmoja kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye kujiandikisha, kugombea katika nafasi mbalimbali na kujitokeza kupiga kura.
“Tusisahau sana na tusichanganye, kati ya uchaguzi unaosimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi, na uchaguzi huu, unaosimamiwa na Wizara yetu ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Tusichanganye. Daftari kuboresha, litaboreshwa daftari la wakazi, ndilo ambalo litatumika kupigia kura, kwa hiyo kila mkazi, ni lazima ajiandikishe. Lakini daftari lile la Tume, linaboresha ….zoezi lile litafanyika mwakani, kati ya mwezi wa pili na wa nne. Lakini zoezi hili ni mahsusi kwa ajili ya uchaguzi wetu wa Serikali za Mitaa, mwezi Novemba 27, 2024”. Amesema Mhandisi Hamsini.
Kwa mujibu ya ratiba ya matukio kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, zoezi la uandikishaji wa Wapiga Kura litafanyika kuanzia tarehe 11 hadi 20 Oktoba 2024 katika Vituo vilivyopangwa.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 13 GN. Na. 574 wakazi wote wenye umri wa miaka 18 au zaidi na waliokidhi masharti ya kisheria wanahimizwa kushiriki katika uchaguzi wa serikali ya mtaa.