Matumaini mapya ujenzi reli ya kisasa Mtwara-Mbambabay

Songea. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ipo katika mchakato wa kufanikisha ujenzi wa Reli ya Kisasa kutoka Mtwara hadi Mbambabay.

Amesema ni kiu ya Serikali kufanikisha hilo ili kuendeleza ushoroba wa Mtwara utakaoiunganisha Tanzania na mataifa mengine jirani.

Ingawa ujenzi huo si mchakato wa muda mfupi, amesisitiza lazima itajengwa kwa kuwa ndiyo dhamira ya nchi.

Amesema hayo leo Jumamosi Septemba 28, 2024 alipohitimisha ziara ya siku sita mkoani Ruvuma.

Amesema tayari upembuzi yakinifu umeshafanyika kufanikisha ujenzi huo, kinachofanywa sasa ni kutafuta fedha ili utekelezaji uanze.

Ameeleza pia anatafutwa mkandarasi atakayefanya kazi hiyo akisisitiza, “ni jambo litakalokwenda taratibu si haraka kiasi hicho.”

Amesema katika ziara amebaini Halmashauri ya Madaba haijakamilisha ujenzi wa mradi wa hospitali, licha ya Serikali kupeleka fedha.

Kutokana na mazingira hayo, ameitaka kutumia fedha za mapato ya ndani ya halmashauri kukamilisha ujenzi huo haraka.

Amesema ziara imemwezesha kukagua na kuona maendeleo na changamoto za Ruvuma ili zitafutiwe ufumbuzi.

“Ziara yangu ilikuwa ya kujionea hali ilivyo na kuwasikiliza wananchi,” amesema.

Samia amesema Serikali ilitoa ruzuku ya mbolea ya Sh83.5 bilioni iliyoongeza matumizi ya mbolea kutoka tani 32,139 hadi 123,049 msimu wa kilimo wa mwaka huu mkoani Ruvuma. Amesema mauzo ya mazao mkoani humo ni jumla ya Sh70.4 bilioni.

Hatua hiyo amesema inapunguza umasikini kwa kiasi kikubwa kwa wananchi, huku akiwasihi kuhakikisha wanatunza fedha walizopata.

Ili kuondoa malalamiko ya wakulima, amesema kuanzia msimu ujao mfumo wa malipo ya mazao ya wakulima iwe moja kwa moja kutoka kwa vyama vikuu vya ushirika badala ya utaratibu wa sasa wa chama kikuu cha ushirika kulipa kwa vyama vya msingi kisha fedha imuendelee mkulima.

Ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha inaongeza ndegenyuki na askari katika vituo mbalimbali ili kudhibiti wanyama waharibifu wakiwemo tembo.

Alirejea msisitizo wake wa mwananchi anayestahili kulipwa fidia baada ya kupisha miradi ya maendeleo atapewa fedha zake.

“Niwasihi wananchi muendelee kupisha ujenzi ili miradi ikamilike na kwamba fedha zikipatikana mtalipwa,” amesema.

Kuhusu utunzaji wa mazingira amesema hekta 100,004 zimefyekwa kwa mwaka mkoani humo.

Amesema hilo linafanywa kwenye mabonde ya mito Luwegu na Pitu na kandokando mwa barabara ya Songea.

Uharibifu kama huo  amesema unafanyika hata katika maeneo ya migodi, huku akilitaka Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufuatilia mara kwa mara migodini.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema kila halmashauri katika mkoa huo imepewa magari ya kubebea wagonjwa.

Amesema tangu Rais Samia alipoingia madarakani takribani magari ya kubebea wagonjwa 500 yamenunuliwa na kila halmashauri mkoani humo imepata gari.

Ameeleza nia ya Rais Samia ya kuhakikisha kila kata inajengwa shule ya sekondari na sasa shule 665 zimeshajengwa.

Katika uongozi wa Rais Samia, amesema nyumba za walimu 366 zimejengwa na madarasa 50,020.

Mchengerwa amesema Rais Samia ameeleza kuongezwa barabara za kiwango cha lami hasa katika maeneo mengi ya Mkoa wa Ruvuma.

Amesema kilomita 23 za barabara kiwango cha lami zitajengwa katika mitaa mbalimbali.

“Watanzania wapo tayari kwenda na wewe kwa hali yoyote, wapo tayari. Watanzania walio wengi hawatarudi nyuma kwa kazi unayoifanya,” amesema.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema hatua ya Rais Samia kuacha safari ya kwenda Marekani kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa, ni ishara ya mapenzi yake kwa wakazi wa Ruvuma.

“Jana (Septemba 27) ulipaswa kwenda nchini Marekani kuhutubia Baraza la Umoja wa Mataifa na ulishauriwa kubadili ratiba ya ziara lakini umekataa. Hii ni ishara ya mapenzi yako kwa wakazi wa Ruvuma,” amesema.

Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo na mbunge wa Songea Mjini, Dk Damas Ndumbaro ameomba vituo vya kununulia mahindi viongezwe ili kuwarahisishia wakulima kuuza mazao maeneo ya jirani.

Pia, ameomba kupata vifaa vya kuchekechea na kusafishia mahindi, kwani mazao yao huwa na vumbi kwa kiasi kikubwa.

Ombi lingine lililowasilishwa na Dk Ndumbaro ni kukarabatiwa kwa barabara kutoka Songea kwenda Makambako.

Dk Ndumbaro amesema ni kiu yao kuona reli inajengwa kutoka Mtwara kwenda Mbambabay.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Abbas Ahmed Abbas ameahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu ya kuhudumia wananchi kwa weledi.

Amesema kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024 watazingatia 4R bila kuathiri ushindi wa kishindo.

Related Posts