Mdamu: Asanteni Wanzania, nimeanza maisha mapya

MWAKA huu, Mwanaspoti liliibua mateso ya miguu ya straika wa zamani wa Polisi Tanzania, Gerald Mathias Mdamu kuvuja usaha jambo lililowagusa Watanzania kujitoa kuhakikisha anapata matibabu.

Katika mwendelezo wa makala, Mwanaspoti lilitafuta msaada wa wataalamu wa afya ili kujua kinachomsumbua lengo likiwa kumsaidia mchezaji huyo kutibiwa.

Mwanaspoti lilimtafuta daktari bingwa wa magonjwa ya mifupa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi), Kennedy Nchimbi aliyemfanyia Mdamu upasuaji wa mwisho baada ya kupata ajali, Julai 9, 2021.

Baada ya kumpata daktari huyo alishauri Mdamu aende ili kuangalia hali yake, na Mwanaspoti likafanya hilo, ndipo alipogundua tatizo na akafanyiwa upasuaji wa paja la kushoto.

Wadau mbalimbali, baada ya kusoma taarifa na kuona video katika mitandao ya kijamii ya Mwananchi Digital walijitoa kufanikisha matibabu na gazeti hili linaendelea kuwajuza hali yake.

Mwanaspoti lilimtafuta Mdamu kwa mara nyingine ili kujua maendeleo kutokana na dawa anazotumia baada ya upasuaji, ambapo anawashukuru Watanzania, madaktari na Mwanaspoti, jinsi ambavyo wamebadilisha maisha yake kutoka kuishi kwa wasiwasi na sasa ana matumaini na amani.

“Kinywa changu hakitachoka kusema asante kwao. Awali nilikuwa naishi kwa wasiwasi, ila kwa sasa naishi kwa matumaini ya kesho. Vidonda vikikauka najua nitakuwa nafanya shughuli zangu za kuitunza familia yangu,” amesema.
 
HALI KWA SASA
Mdamu amesema anaendelea kutumia dawa zinazomsaidia kuvuta uchafu wa ndani utoke nje.

“Pamoja na kutumia dawa nilizopewa nakwenda Hospitali ya Muhimbili kusafisha kidonda maana matundu ya zamani ambayo yalikuwepo paja la mguu wa kulia, kuliota kijipu pembeni kama kilikuwa kinatafuta njia ya kutolea usaha uliokuwa ndani, hivyo kilipasuka,” amesema Mdamu.

“Kidonda hakiwezi kukauka siku moja ndio maana nakwenda hospitali kukisafisha kulingana na maelekezo ya madaktari, ikifika muda nitakaa sawa.”

Mbali na hilo, Mdamu amesema ukikaa sawa mguu wa kulia ambao alifanyiwa upasuaji ataanza kushughulikia suala la kutengenezewa kiatu cha mguu wa kushoto ambao kisigino hakikanyagi chini. 

“Nikijiona nimekaa sawa mguu wa kulia nitaanza kushughulikia kwenda kutengeneza kiatu cha kuvaa mguu wa kushoto. Pia nitaangalia kiasi cha pesa kitakachobaki kama nitaweza kukata bima,” amesema.

LIPA PESA SH3.2 MILIONI
Nje na Sh1.5 milioni ambazo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Rais Wallace Karia lililipa moja kwa moja hospitali kwa ajili ya matibabu, kuna pesa nyingine zilichangwa na Watanzania.

Kuna Sh1 milioni zilitolewa na Mwamnyeto Foundation iliyopo chini ya kiungo wa Singida Black Stars, Zawadi Mauya na nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto ambao walisema zitamsaidia kwa ajili ya chukula na anafanya hivyo kipindi ambacho anaendelea kujiuguza. 

“Pesa ambazo nimetumiwa kwa lipa namba ni Sh3.2 milioni ikiwemo na S 1.5 milioni niliyotumiwa na makamu wa rais wa Yanga, Arafat Haji, ndio maana nataka nikipon, pesa itakayosalia niangalie utaratibu wa kukata bima ya matibabu na kutengeneza kiatu, maana kwa sasa bado naendelea kujiuguza,” amesema na kuongeza:

“Kuhusu mke wangu ameacha kuuza chakula katika mgahawa aliyokuwa anafanya, kuna mdau alituahidi atampatia pesa ya kufanya biashara kwa sasa kasema yupo bize akitulia atafanya hivyo.”

Na kuhusiana na watoto shule anasema: “Ipo vile vile kama mwanzo ambapo mkurugenzi wa shule ile alitupunguzia ada.”

NENO LA MKEWE
Mke wa Mdamu, anayejulikana kwa jina la Juliana amesema kwa sasa anaona mwanga wa mumewe kurejea katika afya yake.

“Sitaacha kuwashukuru Watanzania katika maisha yangu, lakini shukrani ya kipekee ni Mwanaspoti ambalo kila mara lilikuwa linamjulia hali Mdamu na kuwapasha habari Watanzania ambao walijitoa atibiwe, anaendelea na matibabu. Akipona tutarudi tena kuwaambia asante,” amesema Juliana.

Related Posts