Mido Coastal Union aukubali mziki wa Aucho

KIUNGO wa Coastal Union, Gift Abubakar amesema,  mchezaji anayemvutia katika Ligi Kuu Bara ni kiungo nyota wa Yanga, Khalid Aucho.

Gift aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea Proline FC ya kwao Uganda alisema licha ya Aucho kutoka taifa moja ni miongoni mwa viungo bora anaovutiwa na uwezo wake, huku akiweka wazi alipotua nchini aliwasiliana naye kwanza.

“Ni zaidi ya rafiki kwa sababu ni mtu anayenipa ushauri na kiukweli namsikiliza sana. Ananivutia aina ya uchezaji wake na ndio maana nimekuwa nikijifunza vitu vingi kutoka kwake kuanzia namna bora ya uchezaji na nidhamu yake,” alisema.

Akizungumzia tofauti ya  Uganda na Bara, Gift alisema nchi zote ushindani ni mkubwa isipokuwa Tanzania kuna nyota wengi wakubwa na wazoefu na pia ishu ya uchumi mzuri.

“Kwa Afrika Mashariki kiukweli Tanzania imepiga hatua kubwa kwa sababu wachezaji waliopo sio wa kuwabeza. Uganda kuna vipaji vingi sana lakini bahati mbaya ligi ya kule uchumi wake sio mkubwa ndio maana wengi wanaondoka.”

Mbali na kuichezea Proline FC, Gift ameichezea KCCA FC akiwa ni Mganda wa pili kujiunga na Coastal Union msimu huu baada ya beki wa kati, Louis Anguti Amagu aliyetokea KCCA FC.

Related Posts