Moshi. Dainess Shao, mama mzazi wa Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Jonais Shao aliyeuawa kwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana amesimulia alivyokuwa akimsubiri ahudhurie maziko ya baba yake mdogo.
Mauaji hayo yalifanyika Septemba 23, 2024 eneo la msitu wa Hifadhi ya Korogwe Fuel, uliopo Kijiji cha Sindeni wilayani Handeni.
Siku hiyo Jonais (46) alikuwa ametoka Dar es Salaam akapita nyumbani kwake Korogwe ili baadaye aende Moshi kwa maziko ya baba yake mdogo Charles Shao, katika Kijiji cha Maring’a Kondiki, Mwika.
Pamoja na Jonais, wengine waliouawa ni mwanaye Dedan Shayo (8), mwanafunzi wa darasa la tatu na Salha (18), msichana wake wa kazi.
Dainess amesema Jonais ni mwanawe wa kwanza aliyekuwa tegemeo lake baada ya baba yake mzazi, Edward Shao kufariki dunia miaka michache iliyopita.
Akizungumza na Mwananchi wakati wa maziko ya Jonais na mwanaye Dedan yaliyofanyika leo Septemba 28, kijijini Maring’a Kondiki mama huyo amesema Septemba 26, siku ya maziko ya Charles alimsubiri sana mwanaye akiamini atafika lakini hakufika na hakuwa na taarifa kuhusu kilichomsibu.
“Katika mahangaiko yangu, mbona hafiki! mbona hafiki! nikaambiwa amefika Wilaya ya Mwanga, mara yuko hapo, mpaka mahubiri yanaisha nampeleka mashambani kumzika ndiyo napata taarifa kwamba mtoto wangu amekufa kwa kuchomwa moto.”
“Hili tukio linaniumiza, ndugu jamaa na marafiki, majanga jamani! majaribu huku duniani yamezidi hebu angalieni tu hizi dhiki zinavyokuja huku duniani,” amesema akitokwa machozi.
Amesema, “taarifa za kifo cha mwanangu na namna alivyofariki zimenisikitisha sana, maana huyu ni mtoto wangu wa kwanza, ndio lango langu, ndio tegemeo langu.”
Ameviomba vyombo vya dola vichunguze tukio hilo ili mwanaye na mjukuu wake wapate haki zao.
Lameck Shao, mume wa Jonais amesema mara ya mwisho mke wake alikuwa Dar es Salaam na Jumatatu Septemba 23 alikwenda Korogwe ambako njiani waliwasiliana hadi alipofika lakini baadaye hakupatikana tena hadi alipokuja kupata taarifa za kifo chake.
Akisoma historia ya marehemu, Mchungaji Jesse Shao, ambaye ni mwanafamilia amesema walivamiwa nyumbani kwao na watu wasiojulikana na kisha kuondoka nao zaidi ya kilomita 50 ambako walichomwa moto msituni.
Akihubiri wakati wa ibada ya mazishi, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Barikiel Panga amelaani tukio hilo la mauaji akisema hakuna kabila lolote wala dini yoyote inayoruhusu mtu kutolewa uhai.
“Lameck na familia yako endeleeni kuweka tumaini lenu kwa Mungu, ameruhusu jambo hili kutokea. Kama lilivyokuwa kwa machungu na maumivu makubwa ana mipango na maisha yenu, wekeni tumaini lenu kwa Mungu aliye hai yeye atawatunza kadri ya mapenzi yake,” amesema.
Ameitaka jamii kukemea na kuwaombea wale wote wenye tabia za kinyama wakutane na neema ya Mungu ili waache maovu na kuwakatili wenzao.
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 24, kuhusu tukio hilo la mauaji Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi alisema lilitokea Septemba 23, saa tatu usiku.
Alisema Polisi ilipokea taarifa kuwa ndani ya msitu wa Korogwe Fuel kuna gari aina ya Toyota IST lenye namba za usajili T 305 EAL linaungua moto na pembeni yake kuna watu wawili wanaungua.
Kamanda alisema askari walifika eneo hilo na kukuta kuna gari ndogo linaungua moto na pembeni yake kukiwa na watu wawili wameungua kwa moto na kufariki dunia wakiwa pembeni ya gari hilo.
Mchunguzi alisema baada ya uchunguzi wa awali ilibainika miili iliyokuwa nje ya gari ni ya jinsia ya kike na ndani ya gari kiti cha nyuma ulionekana mwili mwingine ambao umeungua moto hadi kupoteza sura na haikuwa imebainika ni wa jinsia gani.