MSHAMBULIAJI wa Fountain Gate, Selemani Mwalimu ‘Gomez’ amesema mwenendo aliokuwa nao katika michezo ya Ligi Kuu Bara hadi sasa unampa morari kuendelea kupambana zaidi, huku akiweka wazi atahakikisha anaendelea kufunga kila akipata nafasi.
Kauli hiyo inajiri baada ya kufunga bao moja juzi katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 3-1 dhidi ya Kagera Sugar na kufikisha manne ya Ligi Kuu Bara msimu huu, akiwa ndiye kinara akifuatiwa na nyota mwenzake, Edgar William mwenye matatu.
“Siwezi kuweka ahadi ya kwamba msimu huu nitafunga mabao mangapi isipokuwa nitahakikisha kila ninapopata nafasi naweza kuzitumia vizuri, siri kubwa ni ushirikiano na wenzangu kwa sababu bila ya wao tusingefika hapa tulipo leo,” amesema.
Nyota huyo amesema kwamba licha ya msimu uliopita kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL), ila sio rahisi kufanya kile alichokifanya na kikosi cha KVZ, kwa sababu ushindani wa Bara na visiwani ni tofauti ingawa ndio malengo aliyonayo.
“Ikitokea itakuwa jambo nzuri kwangu kwa sababu malengo ya mshambuliaji siku zote ni kuona anafunga, Ligi ya Bara ni ngumu sana kwa sababu timu zina wachezaji wazuri na wazoefu, hivyo nitaendelea kupambana zaidi kadri ya uwezo wangu.”
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Mohamed Muya amesema Selemani ni mmoja wa washambuliaji wazuri wazawa ambao wanapaswa kuwatazama kwa jicho la tatu, huku akiweka wazi kuwa siri kubwa ya kiwango chake ni kufuata vyema maelekezo yake.
Selemani amejiunga na kikosi hicho msimu huu baada ya kuachana na KVZ ya Zanzibar ambapo msimu uliopita alikuwa mfungaji bora kutokana na kufunga mabao 20 na asisti saba katika michezo 27 kati ya 30 aliyocheza.