Moshi. Mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi miwili, amekutwa ametupwa katika chemichemi ya Cofee Curing katika mtaa wa Samaria Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, huku akiwa amefariki.
Mwili wa mtoto huyo ulikutwa kwenye maji ukiwa kwenye mfuko, leo Septemba 28, 2024, saa 2:00 asubuhi na mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye alikuwa akitengeneza bomba ambalo lilipasuka.
Akizungumza katika eneo la tukio, askari wa Jeshi la Zima moto na Uokoaji, Sajenti Martine Mapunda amesema walipata taarifa za uwepo wa mtoto huyo kwenye maji asubuhi kutoka kwa mmoja wa wananchi wa eneo hilo, walifika haraka lakini walikuta ameshafariki.
Ametumia nafasi hiyo kuiasa jamii kuepuka kufanya vitendo vya kikatili na kwa wale ambao wanapitia changamoto mbalimbali za kimaisha, watoe taarifa ili wasaidiwe badala ya kuchukua uamuzi mgumu usiostahili katika jamii.
“Tukio hili ni la kikatili, niwasihi wanajamii wanapokuwa na matatizo watafute msaada na si kutupa watoto, tunatambua yapo maeneo ambayo wanaweza kufika na kusaidiwa,” amesema.
Sebastian Mushi, mkazi wa mtaa Samaria ambaye ndiye alitambua uwepo wa mtoto huyo, amesema alifika eneo hilo kwa ajili ya kuziba bomba lililokuwa limepasuka na ndipo alipoona kitu kwenye mfuko.
“Nilikuwa naenda kuziba bomba lililokuwa linarusha maji ndipo nikaona kitu kama mtoto, nikatoka kurudi nyumbani ndipo tukatoa taarifa kwa watu wa zimamoto na uokoaji na mara moja wakafika kumtoa.
“Mtoto huyu anaonekana alitupwa hapo kwenye maji siku mbili au tatu zilizopita, maana tayari alianza kuliwa na wadudu wa kwenye maji,” amesema.
Naye Rose Mushi mkazi wa mtaa wa Arabika ameiomba jamii kushiriki katika kukemea vitendo vya kikatili na kutoa ushirikiano kuwabaini wote ambao wamekuwa wakihusika na vitendo hivyo, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.