Musoma kuchochea uchumi kwa mbio za marathon

Musoma. Wilaya ya Musoma inatarajia kuandaa mbio za Marathon zitakazochochea na kusisimua uchumi wa Manispaa ya Musoma pamoja na watu wake.

Akizungumza leo Jumamosi Septemba 28, 2024, kwenye uzinduzi wa klabu ya michezo yakiwemo mazoezi ya kikimbia (jogging) mjini Musoma Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema mbio hizo zinatarajiwa kufanyika kabla mwaka huu haujaisha.

Amesema tayari maandalizi ya mbio hizo yameanza ikiwa ni pamoja na kuunda kamati maalum ya kuratibu shughuli hiyo ambapo amesema pamoja na uwepo wa fursa mbalimbali za kiuchumi katika Wilaya ya Musoma lakini amebaini uchumi wa mji huo bado haujasisimka hivyo kuhitajika jitihada zaidi hali itakayosaidia ongezeko la mzunguko wa fedha katika jamii.

Amesema mbali na mbio hizo pia ofisi yake imeandaa bonanza maalum la michezo litakaloshirikisha makundi mbalimbali ndani ya Manispaa hiyo wakiwepo watumishi wa umma na binafsi, bodaboda, machinga,viongozi dini wana siasa na makundi maalum.

“Sote tuna kiu ya maendeleo lakini nataka mjue maendeleo yanakuwepo pale penye amani na utulivu na pia tutambue amani na utulivu vinapatikana pale tunapokuwa wamoja, tunaongea pamoja na michezo ni kiungo mojawapo cha kutukutanisha sote  wana Musoma bila kujali itikadi za vyama, imani zetu wala kabila zetu,” amesema Chikoka.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka (mwenye nguo nyeusi) akishiriki mchezo wa kuvuta kamba wakati wa uzinduzi wa klabu ya michezo katika Manispaa ya Musoma. Picha na Beldina Nyakeke

Meya wa Manispaa ya Musoma, William Gumbo amempongeza mkuu huyo wilaya kwa ubunifu wake wa kutumia michezo kuwaleta kwa pamoja watu wa Musoma.

“Nikuombe tu mkuu wangu hili suala liwe endelevu kwani michezo ni afya, michezo ni furaha, michezo ni maendeleo na sisi wana Musoma tunaahidi kukupa ushirikiano,” amesema Gumbo.

Amesema mwitikio mkubwa wa wakazi wa Manispaa ya Musoma kuhudhuria shughuli hiyo ni kielelezo cha utayari wa wakazi wa mji huo kushiriki katika matamasha mbalimbali ya kimichezo.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wamesema kwa muda mrefu wamekuwa na hamu ya kushirki katika michezo na mazoezi kwa ujumla lakini walikosa fursa hiyo kutokana na kutokuwepo kwa mratibu.

“Wengi tunatamani sana kushiriki jatika mazoezi kama haya ya leo lakini hakuna kiunganishi,  hivyo tunamuomba mkuu wa wilaya haya mazoezi yafanyike angalau kila mwezi ili kutuweka sawa kiafya, kiakili, kimwili na kijamii pia,” amesema Erasto Daudi

Joyce Nyangi amemema watu wengi wamejiokeza kushirki kwenye michezo na mazoezi ingawa walipata taarifa ndani ya muda mfupi jambo ambalo linaashiria uhitaji mkubwa wa michezo na mazoezi ya pamoja.

Related Posts