Udhamini wa NMB CDF Trophy wafikia Mil. 245/-, kipute kuanza Oktoba 4

 

BENKI ya NMB imetangaza udhamini wa Sh. Mil. 35 wa msimu wa tisa wa Mashindano ya Gofu ya Mkuu wa Majeshi Tanzania (NMB CDF Trophy 2024), kiasi kinachoifanya benki hiyo kufikisha zaidi ya Sh. Mil. 245 za udhamini katika kipindi chote cha michuano hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

NMB CDF Trophy ni michuano maalum, ya wazi ya kimataifa ya mchezo wa gofu, inayotumika kuadhimisha kuanzishwa kwa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ), ambalo Septemba 1 mwaka huu limetimiza miaka 60, mashindano yakiratibiwa na Klabu ya Gofu Lugalo.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya kutangaza michuano hiyo, Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu, Michael Luwongo, aliishukuru NMB kwa kuendelea kuyabeba mashindano hayo kila mwaka wanaadhimisho ya Kuanzishwa kwa JWTZ Septemba 1, 1964.

Alibainisha kuwa mashindano ya mwaka huu yatakuwa na ushindani mkubwa kutokana zawadi nono ya pesa Sh. Mil. 4 kwa mshindi wa jumla kutoka NMB, pamoja na zawadi ya gari aina ya Toyota Harrier kwa mshindi wa pigo la ‘all in one’ linalotolewa na Kampuni ya Toyota Tanzania ambao ni wadhamini wenza.

“Ni mashindano ya wazi yatakayojumuisha kategori zote muhimu katika mchezo huu, ambazo ni wachezaji wa kulipwa ‘proffesional,’ wachezaji wa ridhaa ‘amature,’ wachezaji wakubwa ‘seniors,’ wachezaji wanawake ‘ladies’ na wachezaji watoto ‘juniors.’

“Hadi sasa tunao jumla ya watoto 45 wa timu zetu za vijana hapa ambao watashiriki, lakini kwa upande wa wachezaji wakubwa, waliojisajili hadi sasa wamefikia 185 na matarajio yetu ni kuona idadi ikiongezeka zaidi hadi Oktoba 4 mashindano yatakapoanza.

Akizungumza katika mkutano huo, Getrude Mallya ambaye ni Mkuu wa Idara ya Wateja Maalum wa NMB, aliishukuru JWTZ na Klabu ya Gofu Lugalo kwa kuendeleza mashirikiano mema na taasisi yake na wao wanajivunia heshima ya kubaki kuwa wadhamini wakuu.

“Tunawapongeza kwa kudumisha michuano hii na mashirikiano baina yenu na sisi na tuko hapa kwa karibia miaka tisa sasa kuhakikisha mashindano haya yanafanyika kwa wetredi kwa siku tatu kama ilivyoelezwa na Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo.

“Tunawashukuru Toyota Tanzania na Mohammed Enterprisess kwa kujiunga kama wadhamini wenza na tunaamini zawadi ya gari kutoka Toyota itachochea ushindani miongoni mwa wachezaji watakaoshiriki NMB CDF Trophy 2024,” alisema Getrude katika hafla hiyo.

“Huu ni muendelezo wa benki yetu kudhamini michezo nchini, kama tulivyofanya katika Michezo ya SHIMMIWI, BAMMATA, na mwaka jana tulisaini makubaliano ya kuongeza ufanisi wa usajili wa Mashabiki na Wanachama wa klabu kongwe za soka za Yanga na Simba.

“Pia tuna kumbukumbu chanya za kuzidhamini timu ya taifa ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars,’ Azam FC, Singida United, timu ya Taifa ya mpira wa magongo na Mashindano ya Mashule,” alibainisha Getrude kuwaambia wana habari katika hafla hiyo.

About The Author

Related Posts