Uzembe wa dereva chanzo ajali iliyoua 12 Mbeya

Mbeya. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,  Wilbert Siwa ametaja chanzo cha ajali iliyoua watu 12 na kujeruhi 23, akisema ni dereva kushindwa kuchukua tahadhari kwenye mteremko na kusababisha gari kuacha njia na kupinduka.

Ajali hiyo ilitokea jana Septemba 27, 202 baada ya gari aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa likitokea Mbalizi kuelekea kwenye mnada katika kijiji cha Jojo, Kata ya Ilembo wilayani Mbeya kuacha njia na kupinduka.

Hii ni ajali ya tatu ndani ya mwezi huu, ikitanguliwa ile ya Septemba 4, iliyohusisha basi la kampuni ya Shari Line iliyoua watu tisa na kujeruhi wengine 18 huko Kata ya Chimala wilayani Mbarali na kampuni ya A-N Classic iliyoua 12 na kujeruhi 44, Septemba 6.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 28, 2024, Kamanda Siwa amesema ajali hiyo ilitokea saa 2:30 asubuhi.

“Dereva alikimbia baada ya ajali, Polisi inaendelea kumsaka wakati majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu katika kituo cha Afya Ilembo.

“Tunatoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama na kuacha kupakia abiria kwenye magari ya mizigo,” amesema Kamanda Siwa.

Katika hatua nyingine, Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Ilembo, Dk Philimon Irungi ameeleza hali ya majeruhi, akisema hadi sasa baadhi ya majeruhi wametawanywa katika hospitali tofauti ikiwamo Ifisi na Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Amesema katika majeruhi hao, 15 walikuwa na hali mbaya baada ya kuumia kifuani, tumboni na miguuni ambapo mmoja amehamishiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya na wengine kupelekwa Hospitali teule ya Ifisi.

“Kati ya majeruhi hao 15 walikuwa katika hali mbaya sana na tayari mmoja amepelekwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya na wengine Ifisi, miili ya marehemu ipo hapa kituo cha Afya Ilembo na imeshatambuliwa na ndugu zao” amesema Dk Ulungi.

Majeruhi waeleza ilivyokuwa

Wiliam Mwashiuya amesema alisikia kelele kabla ya ajali na alipokuja kujitambua aliona gari likidondoka mtoni na kumjeruhi mguuni na kichwani.

“Tulipanda lori, sasa kwenye eneo tulikokuwa tukielekea kukawa na mteremko na kawaida pale huwa abiria wanashuka na tulifanya hivyo, lakini baadaye dereva akasema tupande ndio ikatokea hivyo,” amesema Mwashiuya.

Josephine Kinyata amesema hakujua ajali ilivyotokea kabla ya kujitambua amefikishwa kituo cha afya akiomba Watanzania kuwaombea waliokutwa na ajali hiyo.

“Sielewi ilivyotokea ajali, ila nilijikuta nimefikishwa hapa kituo cha afya. Tunaomba Watanzania wenzetu watuombee,” amesema Josephine.

Related Posts