Dar es Salaam. Waandishi wanane wa Mwananchi ni miongoni mwa washindi waliochukua tuzo
kinya’nga’nyiro cha Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (Ejat), kwa mwaka 2023.
Waandishi hao ni pamoja na Julius Maricha wa Gazeti la The Citizen aliyechukua tuzo mbili za malezi na makuzi ya awali ya watoto na tuzo ya michezo kwa upande wa magazeti.
Wengine ni Hellen Nachilongo (The Citizen) aliyeshinda Utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji, Zourha Malisa (Mwananchi Digital) aliyepata tuzo ya Afya ya uzazi, huku Mgongo Kaitira na Anna Pontinus wa Mwananchi Digital wakishinda kipengele cha Afya.
Wengine ni Pamela Chilongola ameshinda tuzo ya habari za Uchumi, George Helahela wa Mwananchi Digital aliyeshinda tuzo ya Elimu, huku, Jacob Mosenda wa The Citizen akishinda tuzo ya uandishi wa habari za uchunguzi kwa upande wa magazeti.
Mwandishi wa gazeti la Mwanaspoti, Eliya Solomon, naye ameshinda tuzo ya kipengele cha habari za Takwimu.
Mshindi wa jumla katika tuzo hizo ametangazwa kuwa ni Mukrim Mohamed Khamis wa KTV TZ Zanzibar.
Mshindi huyo amekabidhiwa hundi ya Sh3 milioni na Naibu Spika, Mussa Azzan Zungu.
Makundi mengine yaliyoshindaniwa katika tuzo hizo ni utawala bora, kundi la watu wenye ulemavu, habari za utalii na uhifadhi, habari za elimu.
Washindi hao waligawanywa kulingana na vyombo vya habari ambavyo ni magazeti, televisheni, redio na mitandao.
Zungu aita waandishi marekebisho ya sheria
Awali akihutubia katika sherehe hizo, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amewataka wadau wa habari nchini, kuwasilisha Serikalini sheria au vifungu vya sheria visivyokidhi matamanio ya wanahabari ili vipelekwe bungeni kufanyiwa kazi.
Zungu aliyemwakilisha Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema Bunge lipo tayari kuweka mazingira wezesheshi ili wanahabari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, huku akiwahakikishia wadau hao kuwa Serikali ni sikivu na kwamba Bunge litatenda haki ili kukidhi matakwa ya wananchi ambapo wanahabari ni sehemu yao.
Alisema mazingira mazingira wezeshi kisheria ni muhimu katika kuongeza umakini, weledi katika kukuza maadili kwa waandishi wa habari nchini.
“Bunge lipo tayari kuboresha sheria ili kuwa mazingira rafiki na wezeshi ili waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa weledi kwa weledi,” amesema Zungu kwa niaba ya Dk Tulia.
Zungu ametumia fursa hiyo, kuwapongeza waandishi wa habari waliokidhi vigezo vya kuteuliwa kuwania tuzo hizo baada ya kupita katika mchujo wa jopo la majaji lililoongozwa na Halima Sharif.
Katika hatua nyingine, Zungu alisema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayoub Rioba ndiye atakayezindua Jarida la Tuzo na Tuzo Magazine ambayo yanakita katika kuhamasisha umahiri katika sekta mbalimbali Tanzania na nje ya nchi.
Amesema Dk Rioba anatekeleza jukumu hilo, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa.