WATAFITI wa kilimo wamejipanga kuzalisha mbegu za muhogo na viazi vitamu, nchini kwa njia ya haraka kwa kutumia teknolojia ya kitalu tanulu (Tunnel system).
Watafiti hao ni wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kituo cha Ukiriguru jijini Mwanza, ambao wameshiriki mafunzo ya matumizi ya teknolojia hiyo katika uzalishaji wa mbegu, yaliyotolewa na watafiti na wagunduzi kutoka Kituo cha Kimataifa Cha Kilimo cha Kitropiki (CIAT) la nchini Colombia.
Taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa TARI kwenye akaunti ya mitandao ya kijamii, imeeleza kuwa uzalishaji huo utarahisisha upatikanaji wa mbegu kwa wakulima.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mkoa huo ni miongoni mwa ile inayolima zao la muhogo na viazi vitamu kwa wingi; na kwamba moja ya changamoto inayowakabili wakulima ni upatikanaji wa mbegu bora msimu unapoanza.
Kituo cha Kimataifa cha Kilimo cha Kitropiki (CIAT), ni shirika la kimataifa la utafiti na maendeleo, linalolenga kupunguza umaskini na njaa huku likilinda maliasili katika nchi zinazoendelea.
Makao makuu yake yapo jijini Palmira, nchini Colombia na lina wanasayansi watafiti zaidi ya 300.