Azam yabanwa, Singida yarejea kileleni

Timu za Azam na Singida Black Stars zimeshindwa kutamba kwenye michezo yao ya Ligi Kuu Bara leo baada ya kulazimishwa sare.

Azam FC iliyotoka kupoteza mabao 2-0, dhidi ya Simba Septemba 26, ilishindwa kuwika ugenini kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa uliopigwa katika Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma na kukifanya kikosi hicho kutoka sare ya tatu msimu huu.

Kikosi hicho kinachonolewa na kocha mpya Mmorocco, Rachid Taoussi, kilianza Ligi Kuu Bara kwa suluhu mbili mfululizo dhidi Maafande wa JKT Tanzania na Pamba kisha kuzinduka kwa KMC kwa kuichapa mabao 4-0, na kuifunga Coastal Union bao 1-0 kabla ya kuchapwa na Simba.

Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua huku ukitawaliwa na ubabe mwingi kuanzia kwa wachezaji hadi benchi la ufundi, umeifanya Azam kufikisha pointi tisa katika michezo sita, sawa na Mashujaa ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Mashujaa inapata sare ya pili mfululizo baada ya Septemba 21, kufungana mabao 2-2, na  Pamba ikiwa ni ya tatu kwa msimu huu katika michezo mitano iliyocheza, kufuatia kushinda miwili, ikizichapa Dodoma Jiji na Coastal Union.

Tangu Mashujaa ipande Ligi Kuu Bara msimu wa 2022-2023, haijawahi kuifunga Azam FC kwani katika michezo mitatu imepoteza mmoja na kuambulia sare miwili.

Mchezo wa kwanza kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu Bara ulipigwa Novemba 1, 2023 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma ambapo Azam FC ilishinda mabao 3-0.

Mchezo wa pili kwao kukutana wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex zilitoka suluhu Aprili 17, mwaka huu.

Mechi nyingine ya jana mapema, ilishuhudia Singida Black Stars ikibanwa mbavu na JKT Tanzania baada ya kulazimishwa sare ya kwanza msimu huu ya kufungana bao 1-1, katika mchezo uliopigwa saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa CCM Liti mjini Singida lakini ikifanikiwa kurejea kileleni mwa msimamo.

Singida iliyoshinda michezo minne mfululizo ya mwanzo kabla ya sare hiyo, ilipata bao lake kupitia kwa mshambuliaji  Mkenya, Elvis Rupia dakika ya 15 baada ya kipa wa JKT Tanzania, Yacoub Suleiman kuutema mpira na kushindwa kuudaka tena.

Bao hilo liliiamsha JKT iliyoanza kulishambulia lango la Singida na dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza ilipata penalti, baada ya Ismail Aziz Kader kufanyiwa madhambi eneo la hatari na beki wa Singida Black Stars, Khalid Habib Idd ‘Gego’.

Hata hivyo, Hassan Dilunga alikosa mkwaju huo baada ya kupanguliwa na kipa wa Singida, Metacha Mnata.

JKT iliendelea kulisakama lango la Singida na dakika ya 67 ikasawazisha kupitia kwa Wilson Nangu likiwa ni bao la kwanza kwake la Ligi Kuu Bara, tangu asajiliwe msimu huu akitokea TMA FC inayoshiriki Ligi ya Championship.

Matokeo hayo yameifanya Singida kukwea kileleni na pointi 13 sawa na Fountain Gate ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, huku kwa upande wa JKT ikiwa nafasi ya saba katika mechi tano baada ya kukusanya pointi saba.

Related Posts