Barka atwaa tuzo  ya Ballon d’Or

KATIKA usiku uliojaa shamrashamra na vionjo vya burudani, Mtanzania Barka Seif Mpanda, ameandika historia baada ya kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka ya Ballon d’Or of the Champions Dream, huko Hispania.

Tuzo hiyo ilitolewa jana usiku jijini Barcelona, na kuashiria mafanikio makubwa kwa nyota huyo wa klabu ya CF Damm ya Hispania.

Barka Seif, ambaye ameonyesha uwezo wa hali ya juu ndani ya msimu huu, alifanikiwa kuwashinda wachezaji wengine wa kimataifa waliokuwa wakiiwania tuzo hiyo.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Barka alitoa shukrani zake kwa klabu yake, mashabiki wake na familia kwa mchango mkubwa waliotoa katika mafanikio yake.

“Kushinda tuzo hii ni heshima kubwa sana kwangu, si kwa ajili yangu tu, bali kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Ninaamini hii ni chachu ya kuendelea kupambana katika safari yangu,” alisema Barka kwa furaha.

Katika msimu wake akiwa na CF Damm, Barka ameonyesha umahiri mkubwa, akifunga zaidi ya mabao 10 muhimu na kutoa pasi nane za mabao ambazo zimepelekea timu yake kuchukua ubingwa wa michuano ya Champions Dream kwa vijana chini ya umri wa miaka 10. Umahiri wake wa kudhibiti mpira, uchezaji wa kasi, na maarifa kumemfanya kuwa mmoja wa wachezaji wanaotazamwa kama tunu kwenye kikosi hicho.

Mashabiki na wadau wa soka nchini Tanzania wamefurahia ushindi huo wa kihistoria, huku wengi wakiamini kuwa ni mwanzo wa mafanikio zaidi kwa nyota huyo na soka la Tanzania kwa ujumla. “Tuna kila sababu ya kujivunia Barka, ameonyesha kuwa Tanzania ni nchi yenye vipajia,” alisema Omary Mvungi mmoja wa wadau ambao walihudhuria tuzo hizo.

Akimuongelea kijana wake, Seif Mpanda alisema;”Kama mzazi ninafuraha kubwa sana kuona kijana wangu ameshinda tuzo hiyo kwa nafasi yangu nitaendelea kujitoa na kumuombe Mungu aendelee kumfanyia wepesi katika njia zake. Tuzo hiyo ni heshima kubwa familia yangu.”

Kwa ushindi huu wa Ballon d’Or of the Champions Dream, Barka Seif Mpanda anaweka jina lake kwenye orodha ya wachezaji wachache wa Kiafrika waliowahi kushinda tuzo ya aina hii.

Related Posts