Tanga. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kimeiagiza Serikali ya mkoa huo kuchunguza miradi ya maendeleo inayojengwa ambayo kuna dalili za rushwa na kuwachukulia hatua watakaobainika.
Agizo hilo limetolewa leo Septemba 29, 2024 na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdallah wakati akifungua kikao cha kupokea taarifa ya mkoa kuhusu utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2020 – 2025 kwa kipindi cha miezi sita.
Abdallah amesema katika ziara za ukaguzi miradi waliyofanya mkoani humo, wamebaini kuwepo kwa baadhi ya miradi yenye harufu ya rushwa.
Amesema baadhi ya taarifa ambazo walipewa kwenye ukaguzi wa miradi ya afya na elimu waliyopita, kuna maeneo mwongozo wa Serikali wa ujenzi umekiukwa na fedha zimekwisha kabla mradi husika haujakamilika, hivyo lazima ufuatiliaji ufanyike.
Kutokana na hilo, amemwagiza Mkuu wa Mkoa na timu yake kufuatilia miradi hiyo huku akitaja kwamba baadhi ikiwa katika Jiji la Tanga na Wilaya ya Mkinga na ikibainika kuna matumizi mabaya ya fedha za umma, wahusika wote wachukuliwe hatua.
Mwenyekiti huyo ameagiza, pia, kila mtumishi ambaye atabainika kuhusika kwenye uhujumu wa miradi hiyo kwa kujengwa chini ya kiwango, achukuliwe hatua iwe amehama au yupo ndani ya Serikali.
“Tuagize ufanyike ufuatiliaji wa miradi yote ambayo tumekuta ina udhaifu, hatua zichukuliwe, najua mmeshaunda timu kwa ajili kufuatilia hili lakini wote watakaobainika kufanya kinyume na maagizo ya mwongozo wa ujenzi wa miradi, hata kama mtumishi amehama mkoa, arudi na kuchukuliwa hatua,” amesema Abdallah.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa Mkoa wa Tanga, mkuu wa mkoa huo, Balozi Batilda Buriani amesema tayari wamefuatilia baadhi ya miradi na kubaini changamoto mbalimbali katika miradi hiyo.
Amesema wameunda timu kwa ajili ya kufuatilia miradi yote iliyopitiwa na wajumbe wa CCM ili kupata taarifa zaidi kuhusu changamoto ambazo zimetajwa na hatua zitachukuliwa endapo itathibitika kuna changamoto iliyosababishwa makusudi.
Balozi Buriani anasema wamegundua baadhi ya changamoto kuwa ni wananchi hawakushirikishwa, ufuatiliaji mdogo kwa wataalamu miradi katika baadhi ya maeneo, kucheleweshwa kwa fedha na miundombinu ya barabara kuwa sio ya kuridhisha.
Ameongeza changamoto nyingine ni kutokuwa na makadirio sahihi ya vipimo na matumizi mabaya ya fedha za miradi. Ambapo katika maeneo ya miradi na tayari baadhi ya hatua zimeshachukuliwa.
“Na sisi tumewaelekeza watumie vizuri pesa za Serikali zinapoletwa kwenye miradi husika kwa kuepuka matumizi makubwa kuliko kawaida, lakini wahandisi pia waliambiwa kufanya makadirio halisi ya vifaa vya ujenzi ili kuondokana na changamoto zinazotajwa katika miradi yote 47 iliyotembelewa,” amesema Balozi Batilda.
Mjumbe wa kikoa hicho, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava amemuomba Abdallah kuishauri Serikali kuangalia namna ya kufufua mashamba ya chai ya eneo la Bungu wilayani humo, kwani kuna wakulima zaidi 1,810 wanategemea kilimo hicho.
Amesema kwa sasa wanashindwa kuendelea na kilimo hicho baada ya viwanda vya kununua zao hilo kufungwa hivyo kukosa sehemu ya kupeleka bidhaa hiyo.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Mussa Mwanyumbu amesisitiza kuangalia namna ya kutafuta suluhisho la mgogoro kati ya wakulima na wafugaji, kwani jambo hilo limekuwa likisumbua watu wengi.