Dk Nkoronko ataja vipaumbele vitano uongozi MAT

Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko ametaja vipaumbele atakavyoanza navyo katika uongozi wake wa miaka miwili.

Miongoni mwa  vipaumbele hivyo kuwa ni kuchagiza huduma bora na salama kwa wagonjwa, kutumia maarifa, weledi, ujuzi, uzoefu na kuunganisha wanachama.

Dk Nkoronko ameyasema hayo leo Septemba 29, 2024 alipozungumza na Mwananchi, baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo hapo jana.

MAT imemuapisha Dk Nkoronko kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka 2024 mpaka 2026, huku ikimchagua Dk Alex Msyoka kuwa rais mteule jana jijini Dodoma, ambaye atapokea kijiti kwa Dk Nkoronko atakapomaliza muda wake mwaka 2026.

Dk Nkoronko anachukua nafasi iliyoachwa na Dk Deus Ndilanha ambaye ametumikia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili. Dk Deus kwa sasa ataendelea kuwa Mshauri Mkuu wa rais aliyepo madarakani kwa kipindi cha miaka miwili.

Dk Nkoronko amesema katika utendaji wake ataunganisha wanachama na wadau wa sekta ya afya na sekta nyingine.

Pia amesema atahakikisha kwa pamoja wanahamasisha na kuchagiza madaktari kutoa huduma bora kwa wagonjwa na salama kwa ustawi wa afya ya jamii huku wakitumia weledi, maarifa, ujuzi na uzoefu.

“Pia kushiriki kikamilifu katika mipango mbalimbali inayosaidia uzuiaji na udhibiti wa magonjwa. Wajibu wa daktari si kutibu pekee lakini kuondoa magonjwa yanayoweza kuondolewa na kutibu magonjwa yanayozuilika ulimwenguni, lengo kubwa ni kusaidia nchi,” amesema na kuongeza;

“Kusaidia kufanikisha sera, mipango na mambo mbalimbali yanayostawisha sekta ya afya, ustawi wa wanataaluma ili waendelee kutoa huduma bora.”

Dk Nkoronko amesema watatoa mafunzo, tafiti, huduma na watajikita kutimiza majukumu yao kwa manufaa ya afya ya jamii.

“Nchi yetu suala la afya lilipiganiwa kabla ya uhuru, tuliwataka wakoloni waondoke nchi hii ili tuwe na mifumo imara. Tulipopata uhuru, Mwalimu Nyerere alichagua maradhi kama miongoni mwa maadui watatu wa Taifa,” amesema.

Amesema mwisho nchi iliona maboresho makubwa katika sekta ya afya na alipoingia Rais wa awamu ya pili (Ali Hassan Mwinyi), aliyaendeleza.

“Alipoingia Mkapa (Benjamin) alisimamia sana uwezeshaji wa vituo vya afya vya Serikali na ugharamiaji wa huduma za afya na kuchangia, wakati huo ndipo bima ya afya ilizaliwa. Kikwete (Jakaya) akasema tuwe na mpango wa maendeleo ya wa afya ya msingi na hapo ikawa zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata.” amesema.

Dk Nkoronko amesema Serikali ya awamu ya tano ilikuja na uboreshaji wa hospitali kubwa za ubobezi, “Tuliona upanuzi mkubwa na Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani aliweka miundombinu kwa kutumia mikopo na rasilimali nyingine na afya imekuwa ajenda muhimu.”

Amesema hivi sasa wananchi wanahitaji huduma bora, salama, wagonjwa washiriki kikamilifu kupata matibabu yanayostahili  na kuwa na afya bora.

“Kazi yetu ni kuwashawishi watunga sera, watekelezaji wazingatie mipango kadha wa kadha ambayo tunaitamani, lengo ni kuona huduma za afya kwa nchi zinatolewa vizuri,” amesema.

Kwa upande wake aliyekuwa Rais wa MAT mwaka 2020, Dk Elisha Osati amesema Dk Nkoronko ameapishwa kuwa rais mpya wa chama hicho kwa mwaka 2024/2026, huku wakimchagua Dk Alex Elifuraha Msyoka kuwa rais mteule.

Dk Msoka aliyeshinda katika uchaguzi mkuu wa MAT uliofanyika jana Jumamosi, anakuwa rais mteule, ambaye atapokea kijiti cha Dk Nkoronko atakapomaliza muda wake mwaka 2026.

Dk Nkoronko anachukua nafasi iliyoachwa na Dk Deus Ndilanha ambaye ametumikia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili. Dk Deus kwa sasa ataendelea kuwa mshauri mkuu wa rais aliyepo madarakani kwa kipindi cha miaka miwili.

Kulingana na utaratibu wa MAT huwa na rais aliyepo madarakani ambapo kwa sasa ni Dk Nkoronko, rais mteule atakayechukua kijiti baada ya rais aliyepo madarakani kumaliza muda wake wa miaka miwili (ambaye kwa sasa ni Dk Msoka) na rais aliyemaliza muda wake anayebaki kuwa mshauri mkuu wa rais aliyepo madarakani (Dk Deus Ndilanha).

Related Posts