Dosari za kisheria zamnusuru kifungo cha miaka 20 aliyekutwa na meno ya tembo

Arusha. Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Shinyanga imemuachia huru Peter Ndekeja, aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 20 jela alichohukumiwa kwa kosa la kukutwa na meno kamili mawili ya tembo na vipande saba vya meno ya tembo wawili vyenye thamani ya Dola za Marekani 30,000.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kubaini dosari za kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo.

Imeamuru Ndekeja aliyekuwa amehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Meatu katika kesi ya uhujumu uchumi namba 9 ya mwaka 2023, kuachiwa huru kutokana na dosari hizo.

Dosari hizo ni pamoja na Mahakama hiyo ya chini kushindwa kurekodi ushahidi kwa mfumo wa simulizi, hivyo Mahakama Kuu kushindwa kuelewa ni swali gani liliulizwa kupata jibu ambalo liliandikwa na hakimu (aliyesikiliza kesi hiyo).

Nyingine ni upekuzi kufanyika kinyume na kifungu cha 40 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hivyo chochote kilichofanyika ni kinyume na sheria.

Dosari nyingine ambayo iliungwa pia mkono na wakili wa mashitaka katika rufaa hiyo, ni idhini na cheti cha Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kilichotoa ridhaa ya kusikilizwa kwa kesi hiyo katika Mahakama ya chini kuidhinishwa bila kugongwa muhuri.

Hukumu hiyo imetolewa Septemba 27, 2024 na Jaji Ruth Massam, aliyekuwa akisikiliza rufaa ya jinai namba 22200 ya mwaka 2024.

Baada ya kusikiliza hoja za rufaa zilizoungwa mkono na pande zote, Jaji Massam alisema Mahakama hiyo inaunga mkono uwasilishaji wa maombi ya pande zote mbili kwamba Peter aachiwe huru na kwa sababu hiyo ameikubali rufaa hiyo.

Aidha, alisema ni kanuni iliyowekwa vizuri kuwa katika hali nyingine makosa hayo yanaweza kuamriwa kesi kusikilizwa ila katika kesi hiyo hairuhusu Mahakama kufanya hivyo, kwa kuwa pande zote mbili zilikubali mrufani aachiwe huru baada ya kubaini dosari hizo zitaenda kwenye mzizi wa kesi.

“Baada ya kuzingatia kasoro hizo, sioni haja ya kuangalia sababu nyingine za kukata rufaa kwani kutofuata kifungu cha sheria kunatosha kufanya shauri zima na hukumu kuwa batili,” amesema na kuongeza:

“Katika mazingira hayo, nimejiridhisha kuwa hukumu dhidi ya mrufani haikufanywa ipasavyo kwani Mahakama iliyosikiliza kesi hiyo ilishindwa kuona makosa hayo ambayo yanasababisha mshitakiwa ambaye kwa sasa ndiyo mrufani kutotendewa haki.”

Awali katika Mahakama ya Wilaya ya Meatu, Ndekeja alisomewa shitaka la kukutwa na nyara za Serikali ambayo ni meno mawili kamili ya tembo na vipande saba vya meno wawili ya tembo, zenye thamani ya Dola za Marekani 30,000.  

Katika kesi hiyo, alidaiwa kukutwa na nyara hizo za Serikali kinyume na kifungu cha 86 (1) na (2) (b) cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori, vilivyosomwa pamoja na aya ya 14 ya jedwali la kwanza na vifungu vya 57 (1) na 60 (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupanga, Sura ya 200 (EOCCA).

Ilidaiwa Aprili 29, 2023 katika Kijiji cha Sakasaka Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu alitenda kosa hilo, ambapo baada ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, alikutwa na hatia na kuhukumiwa adhabu hiyo.

Katika rufaa hiyo, Ndekeja aliyewakilishwa na Wakili Sululu, alikuwa na sababu mbili ambazo ni Mahakama hiyo ya chini kukosea kisheria kumtia hatiani na kumuhukumu adhabu hiyo, ilihali upande wa mashitaka haukuthibitisha kesi hiyo pasipo kuacha shaka.

Nyingine ni hakimu aliyesikiliza kesi hiyo hakuwa na mamlaka ya kuisikiliza kwani ridhaa na cheti kinachotolewa na DPP hakikupatikana ipasavyo.

Mjibu rufaa (upande wa mashitaka) uliwakilishwa na Wakili Saguya Goodluck.

Akiwasilisha rufaa hiyo, Wakili Sululu alidai kuwa walileta sababu mbili za rufaa lakini wanaacha sababu ya kwanza na kuendelea na hoja ya pili kuwa Mahakama hiyo ilisikiliza kesi hiyo bila kuwa na ridhaa na cheti kilichopatikana ipasavyo.

Alidai kuwa katika shauri hilo, ridhaa ya kesi kusikilizwa inaonekana ila haikugongwa muhuri na kuidhinishwa.

Huku akinukuu mashauri yaliyowahi kutolewa uamuzi na Mahakama ya Rufani, wakili huyo alieleza kuwa ni kanuni kuwa ridhaa na cheti lazima zigongwe muhuri na kupitishwa kabla ya kuwasilishwa mahakamani na kuomba mteja wake aachiwe huru.

Wakili huyo aliomba Mahakama kutoamuru shauri hilo kusikilizwa upya, kwani kwa kufanya hivyo upande wa mashitaka utaziba mapengo kwenye ushahidi na kuwa baadhi ya makosa yaliyofanyika ni utambulisho usiofaa wa vielelezo.

Alidai kuwa shahidi wa kwanza wa mashitaka akiwasilisha ushahidi, alishindwa kubaini kielelezo alichokitoa mahakamani na hitilafu nyingine ilikuwa ni ushahidi haukurekodiwa kwa njia ya simulizi na kuomba mrufani aachiwe huru.

Akijibu hoja hizo, wakili wa mashitaka aliunga mkono rufaa hiyo ya Ndekeja na kukubali kuwa ni kweli cheti na ridhaa vilipaswa kugongwa muhuri na kuidhinishwa lakini hilo halikufanyika.

Wakili huyo alitaja kosa lingine lililofanyika ni wakati wa msako kwani upekuzi huo ulifanyika usiku bila hati ya upekuzi na kibali cha amri ya Mahakama na kuwa bila kibali hicho upekuzi huo ulikuwa kinyume na sheria, hivyo kuungana na wakili wa Ndekeja kuwa mrufani aachiwe huru.

Jaji huyo alianza kwa kusema baada ya kupitia uwasilishaji wa pande zote mbili, mwenendo wa kesi na hukumu, anaona suala kuu la kuondoa rufaa hii ni kama sababu ya pili ya kukata rufaa ni halali au la.

Kuanza na sababu ya pili kwamba ridhaa na cheti havikupatikana vyema pande zote mbili zilikubali kuwa viliidhinishwa lakini havikugongwa muhuri, amesema Mahakama hiyo inaunga mkono hoja hiyo.

Huku akinukuu mashauri mbalimbali ya Mahakama ya Rufani, Jaji Massam amesema ridhaa ni lazima ipitishwe na kugongwa muhuri kabla ya kufikishwa mahakamani.

Kuhusu kutotambuliwa vema kwa vielelezo, Jaji alieleza kuwa upande wa mashitaka una wajibu wa kuthibitisha kwamba nyara ambayo shahidi wa kwanza aliitambua ndiyo aliyokutwa nayo Ndekeja.

“Mahakama hii katika kusoma ushahidi wa Mahakama ya awali hasa katika ukurasa wa 18, 23 na 26, inaunga mkono kuwa Mahakama ya chini ilikosea katika kurekodi ushahidi wa mashahidi,” amesema Jaji.

Kuhusu msako kutokuwa halali, hoja iliyoibuliwa na Wakili wa Serikali, Jaji huyo amesema anakubaliana naye kuwa upekuzi huo ulifanyika kinyume na kifungu cha 40 cha CPA na chochote kilichofanyika ni kinyume cha sheria.

“Kwa kuzingatia kifungu cha 388 cha CPA, makosa ni makubwa sana ambayo hayapendelei Mahakama hii kuamuru kusikilizwa upya na nia ya haki haihitaji kufanya hivyo. Naifuta hukumu hiyo na kuamuru mrufani kuachiliwa mara moja,” alihitimisha Jaji Massam.

Related Posts