RAIS wa Shirikisho la Soka la Cameroon (Fecafoot), Samuel Eto’o ambaye pia ni nyota wa zamani wa Barcelona, Chelsea na Inter Milan, ameeleza umuhimu wa kuboresha nafasi za timu za Afrika katika mashindano ya kimataifa, huku akisema Tanzania inastahili kuwakilishwa na klabu nne CAF.
Eto’o anasisitiza Tanzania na mataifa mengine yenye ligi imara yanapaswa kuwa na timu nne katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Eto’o aliyasema hayo kupitia akaunti yake ya instagram akichati na mubashara na mashabiki na kusema kwa mfumo wa sasa wa upatikanaji wa timu za kushiriki mashindano haya unahitaji mabadiliko. “Nafikiri ni wakati sahihi kubadilisha mfumo wetu,” alisema.
Anashauri kwamba nchi zenye ligi zenye nguvu, kama vile Tanzania, zinapaswa kupata nafasi zaidi kwenye mashindano haya, tofauti na mataifa yenye ligi dhaifu.
Akijadili mfano wa nchi kama Tanzania, Eto’o anasema; “Mataifa kama Afrika Kusini, Congo DR, Senegal, Misri, Algeria, Morocco, Tunisia na Libya, kutokana na kuwa na ligi bora, yanapaswa kutoa timu nne kwenye CAF CL na nyingine nne za CAF CC. Hii itatoa fursa zaidi kwa klabu hizo kuonyesha uwezo wao na kuongeza ushindani.”
Eto’o alisema anadhani mfumo huo utasaidia si tu kuleta ushindani bali pia kuongeza idadi ya mashabiki wanaofuatilia mashindano haya. “Endapo tutatumia mfumo huu utasaidia kuleta ushindani zaidi lakini pia kuongezeka kwa mashabiki,” aliongeza. Hii ni kwa sababu mashindano yenye ushindani yanaweza kuvutia zaidi hisia na ushiriki kutoka kwa jamii.
Akisisitiza umuhimu wa kuboresha soka la Afrika, Eto’o anasema, “Kila bara sasa duniani linapambana kuongeza ushindani katika mashindano yao ya klabu.” Ni wazi kwamba Afrika inahitaji kujitathmini na kujifunza kutokana na mifano ya bara nyingine ili kuimarisha mchezo wa soka.
Zaidi ya hayo, Eto’o anashikilia kuwa Waafrika ni bora kisoka duniani. “Binafsi naamini sisi Waafrika ni bora kisoka duniani kuliko bara lolote lile.”
Kwa kuzingatia alichosema na Eto’o anayeshikia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika Michuano ya Mataifa ya Afrika, akiwa na mabao 18, inamaana kwamba timu nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara zitajikatia tiketi moja kwa moja ya kushiriki katika Ligi ya Mabingwa na tatu Kombe la Shirikisho yani 5, 6 na bingwa wa Kombe la Shirikisho (FA).