Israel yadai kumuua kiongozi mwingine wa Hezbollah

Beirut/Israel. Jeshi la Israel (IDF) limedai kuwa limemuua kiongozi mwingine wa kundi la Hezbollah la nchini Lebanon, Nabil Kaouk, madai ambayo hayajathibitishwa na kundi hilo.

 Kupitia taarifa iliyonukuliwa na Shirika la Habari la Al Jazeera leo Jumapili Septemba 29,2024 IDF imesema imemuua kamanda huyo wa ngazi ya juu huku kukiwa na mapigano yanayoendelea kati ya pande hizo Kaskazini mwa Israel.

Hata hivyo, taarifa hiyo inakuja ikiwa ni siku mbili zimepita tangu IDF imuue kwa shambulio la bomu Katibu Mkuu na miongoni mwa waasisi wa Hezbollah, Sayyed Nasrallah, taarifa iliyothibitishwa jana Jumamosi.

Israel ilitangaza imemuua Nasrallah kwa shambulio la anga juzi Ijumaa wakati wakiwa katika mkutano wa viongozi wa kundi hilo kwenye makao makuu huko Dahiyeh, Kusini mwa Beirut.

Taarifa hiyo kama ilivyochapishwa na Sauti ya Amerika (VOA) imesema kiongozi huyo aliuliwa pamoja na kamanda wa kikosi cha kusini cha kundi hilo, Ali Karki na makamanda wengine.

Wizara ya Afya ya Lebanon imesema karibu watu sita waliuawa na 91 kujeruhiwa kutokana na shambulio hilo la Ijumaa.

Televisheni ya Lebanon imekuwa ikionyesha uharibifu uliotokana na shambulio hilo, huku moshi ukiwa umetanda angani kutoka kwenye majengo yaliyobomolewa.

Wakati hayo yakitokea Jeshi la Lebanon limewataka raia wake kudumisha umoja, huku mashambulizi ya Israel dhidi ya nchi hiyo yakiendelea.

“Amri ya Jeshi inatoa wito kwa raia kulinda umoja wa kitaifa na kutoingizwa katika vitendo ambavyo vinaweza kuathiri amani ya raia katika hatua hii ya hatari na nyeti kwenye historia ya nchi yetu, kwani adui anafanya kazi kutekeleza mipango yake ya uharibifu na kusababisha mgawanyiko miongoni mwa Walebanon,” imeeleza taarifa ya jeshi hilo.

Hata hivyo, kundi la Hezbollah limesema litaendelea na vita dhidi ya Israel ikiwa ni kuunga mkono wananchi wa Gaza na Palestina na kuilinda Lebanon na wakazi wake.

Wakati huohuo, taarifa zimeonyesha maelfu ya watu wakikimbilia Syria, huku hofu ya uvamizi wa ardhini wa Israel ikiongezeka nchini Lebanon.

Imeandikwa kwa msaada wa mtandao

Related Posts