Kocha Tabora Utd aomba muda

KOCHA Mkuu wa Tabora United, Mkenya Francis Kimanzi amesema, anahitaji muda zaidi ili kutengeneza kikosi cha ushindani msimu huu.

Kauli ya Kimanzi inajiri baada ya kikosi hicho kulazimishwa sare ya bao 1-1 jana dhidi ya KenGold ikiwa ni ya pili msimu huu katika michezo sita ya Ligi Kuu Bara aliyoiongoza, baada ya kushinda miwili na kupoteza pia miwili.

“Ligi ni ngumu na kila timu imejipanga vizuri ndio maana ushindani umekuwa mkubwa bila kujali unacheza wapi, bado tuko sehemu nzuri lakini tunahitaji kubadilika, wachezaji wengi hapa ni wageni na wanahitaji muda wa kuzoeana kwa pamoja.”

Kimanzi aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu aliongeza, licha ya mwenendo huo ila anafurahishwa na aina ya uchezaji kwa kila mmoja wao, huku akiweka wazi matokeo mabaya muda mwingine wanayoyapata hayana maana kwamba wanacheza vibaya.

“Tunahitaji hatua kwa hatua kufikia kule ambako tunapahitaji, sio suala la usiku mmoja kuweza kufanikisha hilo ingawa kuna mwanga unaanza kuonekana mbele, tutapambana kadri ya uwezo wetu kwa sababu tuna wachezaji bora wa kutupigania.”

Tabora ilianza Ligi kwa kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Simba na baada ya hapo ikashinda michezo miwili mfululizo ikiipiga Namungo 2-1, kisha ikaichapa Kagera Sugar 1-0, ikatoka suluhu na Tanzania Prisons kabla ya kuchapwa 3-1 na Fountain Gate.

Kimanzi aliyezaliwa Mei 29, 1976, amejiunga na kikosi hicho msimu huu huku akiwa na rekodi kubwa ya kuzifundisha timu mbalimbali za Kenya ikiwamo ya taifa ‘Harambee Stars’, na klabu kama Wazito, Mathare United, Sofapaka na Tusker FC.

Related Posts