Kumekucha CDF Trophy 2024 | Mwanaspoti

MSIMU wa tisa wa mashindano ya Gofu ya Mkuu wa Majeshi Tanzania (NMB CDF Trophy 2024) utaanza Ijumaa ya wiki hii, huku wadhamini wakuu, Benki ya NMB ikitangazwa kumwaga Sh35 milioni.

Mashindano hayo ya siku tatu yatafanyika kuanzia Oktoba 4-6, kwenye viwanja wa Gofu vya Klabu ya Lugalo, jijini Dar es Salaam ikishirikisha wachezaji mbalimbali maarufu wa mchezo huo.

Akizungumza katika hafla ya kutangaza mashindano hayo wikiendi iliyopita, Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu, Michael Luwongo aliishukuru benki hiyo kwa kuendelea kuyabeba kwa mashindano hayo kila mwaka wa madhimisho ya kuanzishwa kwa JWTZ, Septemba 1, 1964.

Alibainisha mashindano ya mwaka huu yatakuwa na ushindani mkubwa kutokana zawadi nono ya pesa Sh4 milioni kwa mshindi wa jumla, pamoja na zawadi ya gari aina ya Toyota Harrier iliyotolewa na kampuni ya Tayota kwa mshindi atakayepiga mpira ukaingia moja kwa moja katika shimo la kiwanja namba 9 “all in one”. 

Getrude Mallya, Mkuu wa Idara ya Wateja Maalum wa NMB, aliishukuru JWTZ na Klabu ya Gofu Lugalo kwa kuendeleza ushirikiano mzuri na taasisi hiyo na wanajivunia heshima ya kubaki kuwa wadhamini wakuu.

“Tunawashukuru pia Toyota Tanzania na Mohammed Enterprisess kwa kujiunga kama wadhamini wenza na tunaamini zawadi ya gari kutoka Toyota itachochea ushindani miongoni mwa wachezaji watakaoshiriki mashindano haya,” alisema Getrude katika hafla hiyo.

Nahodha wa Lugalo, Japhet Masai alisema wachezaji 185 wanatajia kushiriki mashindano hayo na kati yao, wachezaji 45 watakuwa ‘junior’.

“Ni mashindano ya wazi yatakayojumuisha kategori zote muhimu katika mchezo huu, wachezaji wa kulipwa, wa ridhaa, wakubwa (seniors) na wale wa kike na vijana (ladies’ na juniors),” alisema.

Related Posts