BAADA ya kuvuna pointi nne nyumbani, Mbeya City imesema kwa sasa akili zake ni katika mechi ijayo dhidi ya Mtibwa Sugar itakayopigwa Jumamosi ya Oktoba 5, kwenye Uwanja wa Manungu Complex Morogoro, huku ikiahidi kufanya vizuri msimu huu.
Mbeya City iliyoshuka daraja msimu wa 2022-23, ilianza Ligi ya Championship msimu huu kwa sare ya mabao 2-2, dhidi ya Bigman FC zamani Mwadui FC, kisha kuonja ladha ya ushindi kwa kuichapa Mbeya Kwanza bao 1-0, mechi zote ikichezea Mbeya.
Kocha msaidizi wa timu hiyo, Baraka Kibingu alisema, katika mchezo huo wa kwanza na Bigman FC makosa mengi yalionekana eneo la ulinzi waliporuhusu mabao mepesi na washambuliaji kushindwa kutumia nafasi walizopata, ila anashukuru wamefanyika kazi.
“Tunashukuru wachezaji wametekeleza maelekezo na kushinda mechi ya pili, tunaenda kuboresha zaidi maeneo hayo ili mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar tuendeleze ushindi, tunaenda kukutana na timu imara na wazoefu hivyo, ni lazima tujipange vizuri.”
Beki wa timu hiyo, David Mwassa ambaye aliifungia bao pekee katika mchezo na Mbeya Kwanza alisema, malengo yao makubwa kama wachezaji ni kukipambania kikosi hicho kurejea Ligi Kuu Bara, huku akikiri msimu huu ni mgumu ila watapambana.