Songea. Ni saa 144 zinazounda siku sita ambazo Rais Samia Suluhu Hassan amezitumia mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi.
Kwa mtazamo wa wanazuoni, ziara hiyo kwa maneno machache inatafsiriwa kuwa ya maelekezo, utatuzi kero, fursa na matumaini kwa wakulima.
Mtazamo huo wa wanazuoni, unaakisi uhalisia wa mlolongo wa matukio na kauli za Rais Samia akiwa katika ziara hiyo iliyoanza Septemba 23 na kuihitimisha Septemba 28, mwaka huu kwa mkutano mkubwa Uwanja wa Majimaji, Songea Mjini. Ni ziara ya fursa ya maagizo. Kutekelezeka kwa hayo ni neema kwa wananchi wa mkoa huo.
Ukiachana na zawadi nyingi ambazo mkuu huyo wa nchi huzawadiwa anapotembelea maeneo mbalimbali, katika ziara hiyo alipokea zawadi ya Sh1,800 kutoka kwa wanafunzi wa shule ya awali na msingi ya mchepuo wa Kiingereza ya Chief Zulu, jambo alilosema limeugusa moyo wake.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe akizungumza na Mwananchi kuhusu ziara hiyo amesema mbali na uzinduzi na ukaguzi wa miradi, kilichofanyika ni muhimu kwa wananchi na Serikali kwa ujumla.
Umuhimu kwa wananchi unatokana na kile alichoeleza, watanufaika na huduma kutoka katika miradi husika, lakini kwa Serikali imejionea na kujipima nguvu inazotumia katika kuleta maendeleo.
Kwa mtazamo mwingine, Dk Kabobe amesema ziara hiyo imekuwa muhimu hata kwa CCM kujiimarisha kwa kuwavutia wananchi.
“Ziara hii ni muhimu sana kwa CCM pia, sababu imekuwa ni sehemu ya kuendelea kuonyesha yale yaliyoyafanywa kwa wananchi na kuhamasisha kuungwa mkono kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa,” ameeleza.
Ziara hiyo imehitimishwa na kauli ya matumaini kwa wakulima, hasa wa Kahawa kwa kile alichoeleza Rais Samia kuwa kuanzia mwakani Serikali itafanya mageuzi ya mfumo wa mauzo ya kahawa.
Mageuzi hayo kwa mujibu wa Rais Samia, yanahusisha kuondoa utaratibu wa malipo ya wakulima, kupitia vyama vikuu vya ushirika, kisha vyama vya msingi ndipo yawafikie.
Amesema mwakani, mkulima atakayeuza kahawa yake na mazao mengine, fedha zake atazipokea kutoka kwenye chama chake kikuu cha ushirika na haitapita kwingine kokote.
Msingi wa maelekezo yake hayo ni kile alichobinisha, kuna harufu ya kukatwakatwa kwa fedha hizo za wakulima, pia mfumo huo unatengeneza urasimu na kuwachelewesha wakulima kupata haki zao.
Baadhi ya wakulima wamesema hatua hiyo itawafaidisha zaidi na shughuli zao, wakisisitiza utekelezwaji wa hilo ungepaswa kuanza sasa.
“Kwa kuwa wameambiwa mwakani wanatumia muda uliobaki kutukata malipo yetu, ili wafaidishe matumbo yao.
“Yote haya wanayafanya kwa sababu hawajui uchungu wa kulima. Wengi sio wakulima wa jembe la mkono, wanakaa ofisini tu kuelekeza,” amesema Mtutula Mtutula, mkulima mkoani Ruvuma.
Aidha, vitendo vya baadhi ya wakulima kuendelea kuwauzia mahindi walanguzi wanaonunua kwa bei ya chini, ilhali Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inanunua kwa bei nzuri, ni jambo lingine lililomwibua mkuu huyo wa nchi katika ziara yake hiyo.
Akiwasalimia wananchi wa Mbinga Sokoni, Septemba 25, mwaka huu, amewataka wakulima wabadilike na kuacha kuwauzia mazao walanguzi.
Ameijenga hoja yake hiyo kwa ufafanuzi, walanguzi hununua kilo moja ya mahindi chini ya Sh400, huku NFRA imewekwa kununua kuanzia Sh400 na kuendelea, ni vema wakulima wawaepuke walanguzi.
Amesema kuwauzia walanguzi kunawafanya wakulima wasinufaike na shughuli zao, huku akiitaka NFRA kuendelea kusalia eneo hilo, hadi mahindi yote ya wakulima yatakaponunuliwa.
“Serikali imejitahidi kila inapoona kuna changamoto za wakulima inazitatua, lakini wakulima wenyewe nanyi mnapaswa kubadilika,” amesema.
Hakikisho la kulipwa fidia
Hata hivyo, Rais Samia katika ziara yake hiyo, amewahakikishia wananchi wanaopisha miradi ya maendeleo, kulipwa fidia zao.
Ingawa inaweza kuchelewa, amesema Serikali itahakikisha inampa kila mwananchi haki yake anayoistahiki: “Hakuna mradi utakaopita kwa wananchi, Serikali ichukue ardhi bila kulipa fidia za watu.”
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu ombi la Mbunge wa Madaba (CCM), Dk Joseph Mhagama aliyeomba wananchi watakaopitiwa na ujenzi wa barabara ya Makambako walipwe fidia.
Ni ziara ya fursa Songea
Siku sita za ziara hiyo zilitosha kuibua fursa kwa wafanyabiashara wa Ruvuma kwa kujaza vyumba vya nyumba za kulala wageni hasa wilayani Songea, baada ya watu kufurika mkoani humo na hivyo kuibua fursa kwa wananchi.
Sakina Issihaka, mmoja wa wahudumu katika nyumba ya kulala wageni Songea, alisema wateja walizuia vyumba tangu Septemba 20 na wengi wanahisi kuviachia Septemba 29, mwaka huu.
“Hapa vyumba vimejaa, hata nyumba nyingine ya jirani hapo nako vyumba vimejaa, huwezi kupata chumba kwa ugeni huu walivizuia mapema,” alisema Sakina.
Hali ilivyo kwa Sakina ndivyo ilivyo kwa Modesta Zullu aliyasema vyumba vilizuiwa na karibu kila siku wanakwenda wateja kuulizia nafasi lakini zimejaa.
“Tofauti na ugeni huu, huwa vyumba vinakuwepo. Mimi napata wastani wa wateja watano Kati ya vyumba 10 vilivyopo, lakini kwa sasa vyote vimejaa,” alisema.
Hata hivyo, pamoja na ziara hiyo ya Rais Samia, katika Mji wa Songea kulifanywa tamasha la tatu la taifa la utamaduni, ambalo pia lilichochea ongezeko la watu.
Kufungwa kwa tamasha hilo, ndiyo iliyokuwa shughuli ya kwanza ya Rais Samia katika ziara yake hiyo.
Katika ziara hiyo, Rais Samia aliambatana na mawaziri na naibu mawaziri. Wapo waliopewa maelekezo ya utekelezaji kutokana na kero zilizoibuliwa na wananchi, vongozi ama wabunge. Ikiwa maagizo hayo yatetekelezwa itakuwa ni neema kwa wakazi wa maeneo hayo.
Mawaziri waliopewa maelekezo na wakati mwingine walikuwa wakijibu palepale ni, Jumaa Aweso (Maji), Hussein Bashe (Kilimo), Innocent Bashungwa (Ujenzi), Dk Pindi Chana (Maliasili na Utalii) na Mohamed Mchengerwa wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Baada ya kuweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa mradi wa maji Mtyangimbole katika Halmashauri ya Madaba mkoani Songea, Rais Samia alimtaka Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ahakikishe mradi huo unatoa huduma hiyo baada ya miezi mitatu.
Hatua ya kuelekea hivyo, inatokana na uhalisia wa changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo, inayowakabili wakazi wa eneo hilo, waliosema aghalabu hutegemea maji ya visima na mabwawa ambayo si salama.
“Tunachota maji kwenye visima vya watu binafsi, lakini huwa vinakauka kwa hiyo tutakwenda kuchota mabondeni. Hayo ya mabondeni ni machafu na wanatumia wanyama wengine pia,” alisema Zainab Kanyale, mkazi wa Madaba.
Rais Samia alisema kwa kuwa wananchi wameona jiwe la msingi zimewekwa, wamepata matumaini, hivyo kufikia Desemba mwaka huu, Aweso ahakikishe mradi huo unatoa maji.
“Hakikisheni kufikia Desemba mwaka huu maji yanatoka hapa wananchi wale Krismasi huku wanaoga, kwa sababu tumeweka Jiwe la Msingi tumewapa matumaini,” alisema.
Agizo lingine ni kwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliyemtaka ahakikishe kufikia mwakani malipo ya wakulima katika zao la kahawa yanafanywa kupitia chama kikuu cha ushirika, kisha mkulima moja kwa moja.
Sambamba na hilo, agizo lingine lilimlenga Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana aliyetakiwa kuongeza ndegenyuki, vituo na askari wa kudhibiti wanyama waharibifu kwenye mazao ya wakulima wilayani Tunduru hususan tembo.
Tatizo la miundombinu ya barabara ni miongoni mwa maagizo Rais Samia kwa Bashungwa aliyopewa kuhakikisha yanatekelezwa. Ujenzi na ukarabati wa shule, vituo vya afya pamoja na barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) ambazo zipo Tamisemi ni sehemu ya maelekezo aliyepewa Mchengerwa na kutakiwa kusimamia unakamilika kwa kupelekwa fedha kwa wakati.
Bashungwa alisema Serikali ipo katika mchakato wa utekelezaji wa ujenzi wa madaraja mawili ambayo ni Daraja la Mkili lenye urefu wa mita 20 pamoja na Daraja la Mitomoni lenye urefu wa mita 80 ambalo litaunganisha Wilaya ya Nyasa na Songea Vijijini.
“Wanafunzi mvua ikinyesha walikuwa wanasubiri hadi iishe, hata ikiwa siku mbili watoto wanakuwa upande wanashindwa kwenda upande mwingine,” alisema.
Alieleza tayari alishaelekezwa kuhakikisha kabla ya mwaka huu kuisha, kazi hiyo inaanza na kwamba mchakato wa kuanza utekelezaji wa hilo umeanza.
Mradi mwingine aliosema mchakato wa utekelezaji wake unaendelea ni Reli ya Kisasa (SGR) Mtwara-Mbambabay.
Kadhalika, alisema mradi mwingine ni barabara inayounganisha Tanzania na Msumbiji ambapo Serikali itaikarabati kwa kadri inavyohitajika.
Akerwa wanaonyamazia uzushi
Katika ziara yake hiyo, alipotembelea Wilaya ya Tunduru, kuliibuka taarifa katika mitandao ya kijamii zinazomwonyesha mgonjwa akibebwa katika tenga kupelekwa hospitali kutoka Kituo cha afya Mchoteka.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua ya wagonjwa kubebwa kwenye matenga, inatokana na kushindwa kumudu gharama za kukodi gari la kubebea wagonjwa ambazo ni Sh80,000 hadi Sh100,000.
Taarifa hizo zilianza kujibiwa na Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa aliyasema ni uzushi. Aliijenga hoja yake hiyo kwa kufafanua, Tunduru ni moja ya wanufaika wa magari ya kubebea wagonjwa manne kati ya zaidi ya 500 yaliyonunuliwa hivi karibuni.
Si hivyo tu, alisema Wilaya hiyo pia, ni mnufaika wa programu ya M-mama inayowaajiri madereva wa magari binafsi kubeba wagonjwa pale inapotokea gari la kubebea wagonjwa halipo.
Alisema takriban madereva 20 wamesajiliwa na kulipwa fedha kuifanya kazi hiyo, hivyo hakuna uhaba wa gari za kubebea wagonjwa kama ilivyozushwa.
Alipozungumza Rais Samia alionyesha kukerwa na hatua ya viongozi katika eneo hilo, kunyamazia uzushi huo na kusubiri viongozi wa kitaifa wakanushe, huku akiwataka wawe wanatoa ufafanuzi pindi inapojitokeza suala kama hilo ikiwa ukweli wanaujua.
Awajibu wanaomwita muuaji
Ni ziara hiyo mkoani Ruvuma, ndiyo iliyoibua kauli ya Rais Samia dhidi ya shutuma zinazotolewa na wanasiasa hasa wa upinzani, wakimhusisha na matukio ya kutekwa, kutoweka na kuuawa kwa watu.
Rais Samia alitumia hotuba yake katika hafla ya kufunga Kikao cha Mafunzo cha Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa CCM, kuweka wazi, hakuwahi kuua mtu, labda umasikini na giza.
Katika hotuba yake hiyo ya takriban nusu saa, aliipa UWT jukumu la kuwajibu wanaotoa kauli hizo dhidi yake, akiwasisitiza wasihofu kujibu.
Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo alisema ingawa ni sahihi kutoa majibu kwa wanaojenga hoja hizo, pia alisisitiza umuhumu wa changamoto za utekaji kushughulikiwa.
Alieleza kauli dhidi ya Rais zisiaminiwe kuwa yeye ndiye anayehusika moja kwa moja na vitendo hivyo, isipokuwa mamlaka aliyonayo yanafanya baadhi ya watu watupe lawama kwake, akifananisha na msemo ‘ukubwa jalala.’
Katika mazingira hayo, aliwataka UWT wajibu ni sahihi kisiasa, lakini naye anapaswa kuzungumza asiwaache waendelee kumchafua.