Vita Simba, Yanga imeanza kuchangamka

LIGI Kuu Bara inazidi kuchangamka ambapo kwa muda mrefu pale kileleni hujaiona Simba, Azam wala Yanga ikikaa. Fountain Gate na Singida Black Stars zimekuwa zikipishana.

Angalau Simba imewahi kukaa pale juu msimu huu baada ya kushinda mechi mbili za kwanza kabla ya kuanza majukumu ya michuano ya kimataifa ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika, lakini Yanga na Azam bado hazijaonja baridi la kileleni.

Wababe hao wamekuwa washindani wakubwa tangu mwaka 2008 wakati ambao Azam ilianza kushiriki Ligi Kuu Bara. Ushindani wao unakufanya ufikirie jambo moja kubwa kwamba linapokuja suala la kuwania ubingwa, lazima uwatazame wao.

Rekodi zinaonyesha kwamba tangu mwaka 2008 wakati Azam ikianza kushiriki Ligi Kuu Bara, ni takribani misimu 16 sasa ambapo timu hizo tatu pekee ndizo zimefanikiwa kubeba ubingwa. Azam ikichukua mara moja msimu wa 2013-2014, wakati Yanga ikibeba mara 9 na Simba 6. Kabla ya hapo, kuanzia mwaka 2001, Simba na Yanga pekee ndiyo zilikuwa zikibadilishana kombe hilo.

Hiyo inatosha kusema moja kwa moja kwamba watatu hao ndiyo washindani wakubwa wa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ingawa mbele ya safari lolote linaweza kutokea kwa timu nyingine kuingilia vita hiyo.

Kilichotokea msimu uliopita ambapo Yanga ilijihakikishia ubingwa wa ligi zikisalia mechi tatu, huku vita ya Azam na Simba kuwania nafasi ya pili ikiamuliwa katika mechi za kufungia msimu, ndicho kinatarajiwa kutokea msimu huu.

Hiyo inatokana na namna ambavyo timu hizo zilivyoanza msimu huu ambapo jana Jumapili zote zilikuwa uwanjani kila moja ikipambania pointi tatu. Yanga ikiwa nyumbani dhidi ya KMC, Simba ugenini kwa Dodoma Jiji na Azam ugenini kwa Mashujaa.

Kabla ya mechi hizo za jana, msimamo wa ligi ulikuwa ukionyesha Fountain Gate ipo kileleni na pointi zake 13 baada ya kushuka dimbani mara sita, ikifuatiwa na Singida Black Stars yenye 12 na mechi zake tano.

Simba ilikuwa nafasi ya tatu ikiwa na pointi tisa zilizotokana na kushinda mechi zote tatu za kwanza kabla ya jana, huku Azam iliyofungwa na Simba 2-0, ilikuwa nafasi ya nne ikikusanya pointi nane katika mechi tano. Yanga ndiyo timu iliyokuwa na mechi chache zaidi ambazo ni mbili ikiwa imeshinda zote na kupata pointi sita.

Vigo1
Vigo1

Vita ya wababe hao watatu, Azam, Simba na Yanga inatarajiwa kuendeleza tena msimu huu ukizingatia kwamba Azam wana rekodi yao ambayo wamekuwa wakiifukuzia kwa misimu mitatu mfululizo sasa.

Timu hiyo ikiwa chini ya kocha mpya raia wa Morocco, Rachid Taoussi, ina kazi kubwa ya kuzipiku pointi za msimu uliopita ambazo ni 69.

Kazi hiyo inapaswa kufanyika kikamilifu kwani Azam katika misimu mitatu iliyopita imekuwa na mwendo mzuri katika ligi linapokuja suala la kukusanya pointi kwani tofauti yake imekuwa 10.

Takwimu hizo ni kuanzia msimu wa 2021-2022 ambapo ligi ilirejea kwenye mfumo wake wa kushiriki timu 16 kutoka 20 kisha 18. Msimu huo Azam ilishika nafasi ya tatu ikimaliza na pointi 49, kisha 2022/23 ikakusanya 59 ikimaliza tena nafasi ya tatu na 2023/24 zikafika 69 katika nafasi ya pili, hivyo kwa mwendo huo, kuna deni la kufikisha pointi 79 msimu huu.

Ikiwa timu inatakiwa kucheza mechi 30 zenye jumla ya pointi 90 huku Azam katika mechi 5 za kwanza ikikusanya pointi 8 kati ya 15, ili kuzifikia pointi 79 msimu huu haina budi kupambana kuhakikisha mechi 25 zilizobaki haifanyi makosa. Ikitoboa mechi hizo 25 kwa kushinda zote itakusanya pointi 75 ukiweka na 8 ilizonazo zinakuwa 83, hivyo inavuka malengo. Je, wataweza, tusubiri mbele safari tuone.

Rachid Taoussi, amesema taratibu anawafahamu wachezaji wake hivyo siku hadi siku kile anachokitaka kitaanza kuonekana uwanjani.

“Ili uwe bingwa na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa lazima ushinde mechi zako, tunalifanyia kazi hilo,” alisema Taoussi.

Simba yenyewe msimu huu moto ilioanza nao unawapa matumaini kwani timu hiyo kabla ya jana ilikuwa imeshinda mechi tatu za kwanza kwa kufunga jumla ya mabao tisa huku nyavu zao zikiwa hazijatikiswa.

Kocha Fadlu Davids amekabidhiwa jukumu la kuliongoza jahazi la timu hiyo huku akionekana kuanza vizuri licha ya kwamba alikutana na joto ya jiwe kwenye Ngao ya Jamii alipopoteza Kariakoo Dabi kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga hatua ya nusu fainali kabla ya kurekebisha makosa na kumaliza nafasi ya tatu ikiifunga Coastal Union.

Fadlu ana jukumu zito la kuhakikisha Simba msimu huu inaumaliza utawala wa Yanga katika Ligi Kuu Bara kwani watani zao hao wa jadi wamebeba ubingwa misimu mitatu mfululizo na wakipania kubeba tena msimu huu.

Simba ambayo nayo iliweka utawala wake kwa misimu minne mfululizo kuanzia 2017-2018 hadi 2020-2021, inataka kurudia katika makali hayo msimu hu una jukumu hilo ameachiwa Fadlu.

“Kuna wakati inatokea kuna mechi mfululizo, tunapaswa kukabiliana nazo ili tusitoke kwenye malengo, katika kusaka matokeo siangalii rekodi za nyuma kwa sababu rekodi hazichezi bali kipyenga kinapopulizwa pale mechi ndiyo inaanza na zikitimia dakika dakika tisini matokeo yataonekana. Kikubwa tunajipanga kushinda kila mechi,” alisema Fadlu.

Yanga nao hawapo kinyonge, tayari imeutafuna mfupa wa mechi mbili za ugenini kwa kuzichapa Kagera Sugar (0-2) na KenGold (0-1), jana ilikuwa nyumbani kupambana na KMC ambayo msimu uliopita timu hiyo iliichangia Yanga pointi sita katika kampuni yake ya ubingwa kutokana na kufungwa mechi zote mbili. Ile ya kwanza Yanga ilishinda 5-0, kisha mzunguko wa pili ikashinda tena 3-0.

Miguel Gamondi anayeinoa Yanga, katika kufanikisha malengo yake ya msimu huu, kipindi cha usajili wa dirisha kubwa ameongeza maingizo machache ya wachezaji ambayo kwa asilimia kubwa yameanza kumpa matunda mazuri.

Chadrack Boka, Prince Dube na Clatous Chama ni miongoni mwa wachezaji wanaoanza kikosi cha kwanza wakiwa ni maingizo mapya. Pia kuna Duke Abuya ambaye naye akipewa nafasi huwa hafanyi makosa.

Nyota wa Yanga wanafahamu kwamba wana kazi kubwa ya kufanya msimu huu kutetea ubingwa wao huo, pengine wamepata nguvu baada ya kuchukua Ngao ya Jamii, taji ambalo msimu uliopita lilibebwa na Simba.

Gamondi tangu msimu uliopita amekuwa na mwendo mzuri na vijana wake wakishusha vipigo vikubwa bila ya kuangalia ni timu ya aina gani kwani waliifunga Simba 5-1, KMC na JKT Tanzania zilichapika 5-0 kila moja.

Msimu huu mechi mbili za kwanza za ligi Yanga licha ya kushinda, lakini mashabiki kama hawajaridhika kwani walishazoea kuona mabao mengi.

Gamondi ameatuliza kwa kuwaambia: “Ninapenda kuona tunafunga mabao lakini sio malengo yangu kusema nataka kila siku tufunge mabao mengi.

“Tunatengeneza nafasi nyingi za kufunga, ukiangalia kwa wastani kila mechi tunapiga mashuti zaidi ya 15, wakati mwingine tunafunga bao moja, muhimu kwangu ni pointi tatu na huwa naridhishwa na uchezaji wa timu yangu.”

Vigo2
Vigo2

Rachid Taoussi wa Azam, Fadlu Davids (Simba) na Miguel Gamondi (Yanga), kila mmoja amepewa kazi ya kufanya na mabosi wao wakati msimu unaanza.

Taoussi na Fadlu ni wageni katika soka la Tanzania wakianza kuzinoa timu zao kwa mara ya kwanza msimu huu, lakini Gamondi ni mwenyeji kidogo kwani alikuwepo hapo tangu msimu uliopita.

Ikiwa kila mmoja hapo hesabu zake ni kubeba ubingwa, ni wazi wataonyeshana ubabe mkubwa ndani ya uwanja na tayari tumeona Fadlu akimzidi kete Taoussi walipokutana katika Mzizima Dabi Septemba 26 mwaka huu Simba ikishinda 2-0 dhidi ya Azam.

Oktoba 19 mwaka huu, Fadlu ana mtihani mwingine kwa Gamondi, baada ya mara ya kwanza katika Ngao ya Jamii kupasuka, safari hii ana cha kujiuliza watakapokutana kwenye mchezo wa kwanza wa ligi.

Ilishuhudiwa msimu uliopita Gamondi akiichakaza Simba nje ndani ilikuwa na makocha wawili tofauti, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyebebeshwa zigo la mabao 5-0 na Abdelhak Benchikha aliyepunguziwa dozi na kupokea kichapo cha 2-1. Msimu huu Fadlu ameanza na kichapo cha 1-0 katika Ngao ya Jamii.

Pengine Oktoba 19 tutashuhudia picha nyingine tofauti kuuelekea ubingwa wa ligi msimu huu baada ya matokeo ya mchezo huo. Kumbuka wanapokutana wakongwe hao haijawahi kuwa mechi rahisi.

Vigo3
Vigo3

Ugeni wa makocha hao wawili, Taoussi na Fadlu, inaweza kuwa faida kwa Gamondi kuendeleza kufanya vizuri kutokana na kikosi chake kukaa nacho kwa muda mrefu.

Ukiangalia hata wakati anakiboresha, ameingiza wachezaji wachache ambao ni saba, huku kati ya hao, huku watatu wakiwa wanajitafuta ambao ni kipa Khomeny Abubakar, kiungo Aziz Andabwile na mshambuliaji Jean Baleke.

Gamondi amekizoea kikosi chake, anafahamu vizuri sana ubora wa mchezaji mmojammoja na hata wapinzani wengi anaokwenda kukutana nao anawafahamu.

Hilo alilibainisha wakati anakwenda kucheza dhidi ya Kagera Sugar aliposema: “Msimu uliopita mchezo wa kwanza tulikwenda kucheza dhidi ya Kagera nikiwa siifahamu vizuri, tukapata sare, lakini baada ya kucheza nao mara mbili nimeifahamu ni timu ya aina gani ninayokwenda kukabiliana nayo.”

Gamondi kwa kudhihirisha anaifahamu vizuri Kagera, ameenda Kaitaba ambapo mara ya mwisho alipata matokeo ya 0-0, safari hii ameondoka na ushindi wa mabao 2-0.

Fadlu na Taoussi wanaweza kuteseka kidogo na ugeni wao kwa sababu ya kutozifahamu vizuri timu wanazokwenda kukutana nazo lakini pia wachezaji wao vikosini wote wamekutana wageni.

Taoussi amekuja Azam timu hiyo ikiwa imekamilisha usajili na ishacheza mechi moja ya ligi, Fadlu licha ya kuwa na vijana wake kambini nchini Misri kipindi cha maandalizi ya msimu, lakini ana kazi ya kuweka muunganiko kwa sababu kuna maingizo mapya 15.

Mdogomdogo Fadlu anaendelea kuzoeana na wachezaji wake huku pia akiingiza mifumo yake ili kupata kitu bora zaidi. Wakati wenzake wakifanya hivyo, Gamondi ni kama hana kazi kubwa ya kufanya kwa sababu mengi ameyafanya msimu uliopita kipindi ndiyo kwanza anaanza kuifahamu Yanga. Sasa hivi anateleza tu.

Vigo4
Vigo4

Azam imeumaliza mwendo kimataifa hatua ya awali, Simba na Yanga zipo hatua ya makundi zikisubiri ifike Oktoba 7 ziwafahamu wapinzani wao pindi droo itakapochezeshwa.

Yanga inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Simba ikiwa Kombe la Shirikisho Afrika.

Huko kimataifa Simba na Yanga wana vita yao nyingine ambayo ni kufanya vizuri zaidi ya mwenzake licha ya kushiriki mashindano tofauti.

Msimu uliopita tulishuhudia timu hizo zote zikitinga makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, zikafanya vizuri lakini safari yao ikaishia robo fainali kila mmoja akitolewa kwa staili yake.

Simba ilifungwa na Al Ahly jumla ya mabao 3-0 baada ya mechi mbili za nyumbani na ugenini, wakati Yanga ikitolewa kwa penalti 3-2 dhidi ya Mamelodi Sundowns kutokana na matokeo ya jumla kuwa 0-0.

Simba malengo yao makubwa msimu huu ni kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na tayari Fadlu analifahamu hilo, katika mpango kazi wake ameliweka.

Malengo hayo yamekuja baada ya kuangukia kwenye mashindano hayo huku msimu uliopita walipokuwa Ligi ya Mabingwa Afrika walihitaji kucheza nusu fainali kutokana na mara kwa mara kuishia robo fainali. Kumbuka Simba imetinga makundi kimataifa kwa mara ya sita.

“Malengo makubwa ya timu ni angalau kucheza fainali ikiwezekana kuchukua ubingwa, wachezaji wanalifahamu hilo na tunalifanyia kazi,” alisema Fadlu akiwa anasubiri kuwafahamu wapinzani wake hatua ya makundi.

Yanga wamekuwa wakisema kila mara kwamba wanahitaji kwanza kuizoea hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kisha misimu ijayo huko ndiyo wapange malengo makubwa zaidi.

Tangu waanze kusema hivyo, wamecheza hatua ya makundi katika michuano hiyo mara mbili mfululizo tena yote chini ya Gamondi, msimu uliopita walipofika hadi robo fainali na msimu huu.

Mabosi wa Yanga wanaamini kwamba, timu hiyo kuingia makundi kwa sasa ni mafanikio makubwa kwani kabla ya msimu uliopita, walikuwa wakiifukuzia rekodi hiyo kwa takribani miaka 25.

Related Posts