Wagonjwa walia maumivu gharama za matibabu ya moyo

Dar es Salaam. “Nilipojisikia vibaya na kupelekwa hospitali ya Amana waliniambia kutokana na umri wangu nasumbuliwa na presha na sukari, hivyo walianza kunipa dawa za kutibu matatizo hayo.”

Hiyo ni simulizi ya Zena Abdalla (65) alipozungumza na Mwananchi leo Septemba 29, 2024 katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini hapa.

Amesema ametibiwa maradhi ya presha na sukari kwa muda mrefu, ambapo mwaka 2020 daktari alimwambia apime Uviko-19 kwa kudhani amepata maambukizi ya ugonjwa huo.

 “Baada ya majibu ya vipimo kurudi, walibaini sina maambukizi ya corona waliniambia niendelee kutumia dawa za presha na sukari ndipo nilipovunja ukimya kwani niliona hali yangu inazidi kuwa mbaya kila kukicha,” amesema.

Amesema aliwaambia madaktari hawezi kutembea hatua ndefu, anabanwa na pumzi hivyo anahitaji vipimo zaidi, ndipo Agosti 2024 amegundulika ana tatizo kwenye moyo na kupewa rufaa ya Muhimbili.

“Majibu yalionyesha moyo wangu umetanuka, lakini madaktari waliniambia imesababishwa na sukari na presha hivyo niendelee kutumia dawa,” ameelezea na kuongeza;

“Walipoona hali haibadiliki ilibidi wanipe rufaa ya kuja Muhimbili ambako nilipimwa na kukutwa mirija mitatu inayopeleka damu kwenye moyo imeziba, hivyo natakiwa kufanyiwa operesheni,” amesema.

Hata hivyo, amesema alijikuta anatumia gharama kubwa za matibabu kwani kila alipohudhuria kliniki alitakiwa kulipia Sh110,000 kila mwezi, huku akihitajika kulipa Sh8 milioni kwa ajili ya kufanyiwa operesheni.

Pia amesema kutofanyiwa vipimo vya moyo mapema, kuliliongeza tatizo na limekuwa kubwa, huku akitoa rai kwa madaktari kuwafanyia vipimo zaidi wagonjwa wanaoonekana kuwa na maradhi yasiyopona ili tatizo litatuliwe mapema.

“Madaktari wawe wanaangalia kwenye upimaji, kama ugonjwa mmoja hauponi kwa wakati huo waangalie na vipimo vingine. Mimi nimepoteza muda mwingi kutibu tatizo ambalo lilizalishwa na ugonjwa mwingine,” amesema.

Naye, Erick Lesilwa (24) kutoka kijiji cha Mpunguzi, Dodoma alipatwa na mshtuko alipogundulika kuwa na tatizo la moyo, baada ya kuwa na  alizodhani ni ugonjwa wa kawaida.

Kijana huyo, ambaye alikua akifurahia kushinda juani, alianza kusumbuliwa na maumivu ya kifua na kuishiwa na pumzi mara kwa mara mwaka 2016.

Kwa muda mrefu, alidhani ni hali ya kawaida inayosababishwa na kazi za nje au uchovu. Hata hivyo, hali hiyo ilipozidi kuwa mbaya, familia yake ilimpeleka kwenye kituo cha afya cha kijiji chao.

“Nilipopelekwa zahanati nilikuwa napewa dawa za kumeza kwa kufikiri ni magonjwa ya kawaida kama Malaria, lakini nikirudi nyumbani hali ilikuwa mbaya zaidi na niliporudishwa tena nikapewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Mkoa wa Dodoma,” amesema.

Baada ya vipimo waliamua kumpa rufaa ya kufika Muhimbili na baada ya vipimo walimuhamishia JKCI, ambako aligundulika kuwa mishipa inayopeleka damu kwenye moyo imeziba.

“Baada ya kufanyiwa matibabu hapa niliandikiwa dawa za kumeza lakini kutokana na uwezo mdogo nilishindwa kumudu kuzinunua na kusababisha tatizo hilo kurudi tena na kurudishwa tena hapa hospitali,” amesema Erick.

Amesema familia wamemkatia bima lakini ni ndogo, ambapo wamejikuta kulipia kwa fedha taslimu, kwani gharama za kutibiwa kuzibua mirija ni kubwa.

Mkurugenzi Mtendaji JKCI, Dk Peter Kisenge amesema gharama za kuzibua mirija inayopeleka damu kwenye moyo ni kubwa ambayo ni Sh6 milioni huku ufanyaji wa operesheni ni kuanzia Sh8 milioni hadi Sh15 milioni.

“Ndugu wananchi tumieni nafasi hii kujilinda na magonjwa ya moyo yanaleta umasikini kwenye familia kwa sababu matibabu yake ni gharama, unapopata tatizo la mirija kuziba ili tukufungue pale taasisi ya moyo gharama yake ni Sh6 milioni,” amesema Dk Kisenge.

Amesema kufanya mazoezi hakuna gharama hivyo ni maamuzi ya mtu mwenyewe ikiwemo uzingatiaji wa lishe bora, kujizuia unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara kupita kiasi.

Pia, amewataka wananchi kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara au angalau mara moja kwa mwaka ili inapogundulika ana changamoto aanzishiwe tiba mapema, kwani wengi wao wanajigundua tatizo likiwa kubwa.

Akielezea kuhusu takwimu amesema kumekuwa na ongezeko la magonjwa ya moyo zaidi ya watu milioni 20 kwa mwaka duniani kote, ambapo asilimia 80 wamepata mshtuko wa ghafla wa moyo.

Amesema mpaka sasa wamezunguka mikoa 16 na wameona wagonjwa 17,000 na kati ya hao asilimia 25 walikuwa wana matatizo ya moyo huku asilimia 9 wakiwa hawajui kuhusu afya zao.

“Kwa hapa nchini kwetu asilimia 13 wana magonjwa ya moyo, tunapopita mawodini asilimia kubwa ya wagonjwa tunaowaona wengi wanakuwa na magonjwa yasiyoambukiza, kama vile moyo, kisukari na shinikizo la juu la damu pamoja na kiharusi,” amesema Kisenge.

Related Posts