Nzega Vijijini. Uhaba wa shule za sekondari katika kata ya Isagenhe unawalazimu wanafunzi kutembea hadi kilomita 40 kusaka elimu, huku changamoto hiyo ikitajwa kuwa kichocheo cha utoro.
Changamoto hiyo ya umbali haiishii kwenye utoro pekee, inatajwa kukwamisha ndoto za wanafunzi wengi kuhitimu kidato cha nne, ikielezwa wengi wao huishia njiani wanapokuwa kidato cha kwanza na wengine huishia kidato cha pili na wa kike kuolewa.
Katika kata hiyo iliyopo Wilaya ya Nzega Vijijini, ina shule moja ya sekondari ya Isagenhe iliyopo kijiji cha Buhulyo ambayo inahudumia pia wanafunzi kutoka vijiji vya Zigimlole, Kidete na Rhuhumbo.
Mkuu wa shule hiyo na mwenyekiti wa umoja wa wakuu wa shule za Nzega vijijini, Jumanne Shabani anasema changamoto ya umbali imechangia wanafunzi kuacha shule na baadhi ya wazazi kuitumia kama fursa kuwaozesha mabinti katika umri mdogo.
“Wengi wao huwa hawaji shule sababu ya changamoto hii, hapo ndipo wazazi wanaitumia nafasi hiyo mabinti katika umri mdogo kwa kisingizio kwamba wamekataa shule,” anasema.
Akizungumzia umbali huo, Shabani anasema kuna baadhi ya watoto wanatembea kilomita 20 kwenda shuleni na kilomita 20 kurudi nyumbani kila siku za shule hasa wale wanaotokea kijiji cha Kidete.
“Njiani kuna bonde ambalo nyakati za masika linajaa maji na kusababisha usumbufu kwa wanafunzi wanaotoka eneo hilo kuja shuleni.”
“Inafikia hatua wanachoka, mtoto anakataa shule, ukimhoji anasema kweli hataki, mazingira yanamlazimisha kuacha na mzazi kwa kuwa alitaka hivyo kutokana na mazingira aliyokuwa akimhudumia mtoto wake, anafurahia lengo lake kutimia huku akiwa amejitoa kwenye jambo hilo kwa kisingizio mtoto mwenyewe ndiye hataki,” anasema.
Mkuu huyo wa shule anasema asilimia 20 ya wanafunzi wa Isagenhe wamekuwa wakiacha shule kwa changamoto ya umbali hasa wa kidato cha kwanza na baadhi huachia kidato cha pili.
“Wavulana wanaacha mapema zaidi, wasichana huwa wanaendelea kuwepo lakini mahudhurio yao yanakuwa ya kusuasua na hata kisaikolojia wanakuwa hawapo sawa, ingawa wengi wa wanaomaliza hata ufaulu hupungua mfano ni mtihani wa Moko wa mkoa, wilaya yetu yenye shule 36 ilishika nafasi ya pili kutoka mwisho katika wilaya nane za mkoa wa Tabora,” anasema.
Mradi wa Baiskeli wasaidia
Mkuu huyo wa shule anasema jukwaa la Mtandao wa Kupinga Ndoa za Utotoni wenye mashirika 87 umewasaidia wanafunzi hususani mabinti kurejesha morali ya kusoma tena.
Anasema Shirika la Msichana Initiative lilianza kutoa vifaa mbalimbali vya shule kwa wanafunzi na kuja na mradi wa baiskeli moja msichana mmoja, ambazo ziliwasaidia wasichana kwenda shuleni na kupunguza changamoto ya umbali.
Mtandao huo ambao msimu huu unafanya msafara (Caravan trip) kwenye mikoa minne ya Mara, Shinyanga, Tabora na Dodoma inayoongoza kwa ndoa za utotoni nchini ukiongozwa na mashirika yake sita ya Msichana Initiative, Medea, Plan İnternational, My legacy, Binti Makini Foundation na Theatre Arts Feminist Group unatoa elimu kwa jamii kuhusu athari ya ndoa za utotoni katika mikoa hiyo na Septemba 28, 2024 ulitoa elimu kwenye kata hiyo.
Mtandao huo tangu mwaka 2012 unapaza sauti kupinga vitendo vya ukatili ikiwamo ndoa za utotoni huku ukitaka sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 13 na 17 kibadilishwe ili kumaliza janga hilo.
“Jukwaa hili limetusaidia sana hapa Nzega Vijijini, kwani mila za eneo hili zinamjenga mtoto wa kike kuwa mama na si kumpa elimu, uwepo wa jukwaa hili umeisaidia jamii kuanza kubadilika,” anasema mkuu huyo wa shule akitolea mfano mwaka 2017 mabinti waliohitimu kidato cha nne shule ya Isagenhe walikuwa wanne.
“Mwaka jana mabinti 24 walihitimu na wavulana 20, hii ni hatua kwenye changamoto ya utoro tumetoka sasa tunapambana na ufaulu kwa kuazimia kuweka kambi za masomo kwa madarasa ya mitihani,”anasema.
Ofisa Uchehemuzi wa Shirika la Msichana Initiative, Jacob Maduki anasema wamefanya miradi mbalimbali nchini tangu mwaka 2012 na wilayani Nzenga wamefanya miradi sita katika kata 10 za wilaya hiyo wakipaza sauti kupinga ukatili sanjari na kuwajengea uwezo mabinti kuhusu athari ya ndoa za utotoni.
“Tumekuwa tukiijengea jamii uwezo na hasa kuhusu kuipinga sheria ya ndoa, leo (Septemba 28) tupo Isagenhe kuzungumza na jamii na kupata maono yao kuhusu mila na desturi potofu ambazo zinasababisha watoto wengi hapa wasisome na kuozwa na namna ya kukabiliana nazo,” anasema.
Mmoja wa wazazi katika kata ya Isagenhe, Rehema Mwakinandi anasema eneo hilo lilikuwa na changamoto ya mimba na ndoa za utotoni.
“Miaka ya karibuni familia nyingi zimeanza kuelimika na mabinti kuwa na mwamko wa kusoma, changamoto imebaki ni umbali hadi kuifikia shule, japo baadhi ya mabinti walipata msaada wa baiskeli lakini nguvu zaidi inahitajika na Shirika Msichana Initiative na Mtandao wa Kutokomeza ndoa za utotoni upewe sapoti zaidi ili kutufikia kwa ukubwa zaidi,” anasema.