Kondoa. Ubaguzi wa kutowapeleka watoto wa kike shuleni unaofanywa na baadhi ya wanaume katika kijiji cha Mnemia, Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, umewasukuma wanawake kuanzisha kikundi cha uzalishaji mali ili kuwakwamua na changamoto hiyo.
Kutokana na kukosa mtaji, kikundi hicho kinachojulikana kama Subira, kilichoanzishwa mwaka 2010 kwa kutegemea mapato yanayotokana na uimbaji kabla ya kuingia katika shughuli za mazingira na ufugaji wa nyuki.
Kudra Shamroy ambaye ni mwenyekiti na muasisi wa wazo la kuanzisha kikundi hicho, amesema unyanyasaji wa wanaume katika kutoa elimu sawa kwa watoto wa jinsia zote ndio uliomfanya kuwashawishi wenzake kuanzisha kikundi hicho.
“Baba (mumewe) alikuwa anatoa kipaumbele kwa mtoto wa kiume na kumuacha wa kike nyumbani, kwa madai kuwa ataolewa. Kitendo hiki kiliniuma binafsi, nikatafuta wenzangu, nikawauzia wazo kuwa wanaonaje wamama tukiwa na mradi wetu utakaotuingizia kipato?” amesema.
Amesema bahati nzuri wazo hilo lilikubalika na kwa kuwa hawakuwa na mradi wa kuwawezesha kupata kipato, waliamua kutumia sauti zao kama mtaji kwa kuanzisha kikundi cha kuimba.
Amesema kikundi hicho kilianza na wanawake 11 na wanaume saba na kuwa walikuwa wakiimba nyimbo za kuelimisha kuhusu malaria, Virusi vya Ukimwi na ugonjwa wa Ukimwi na wanapohitajika katika shughuli yoyote walikwenda.
Hata hivyo, unyanyapaa uliwafanya wanaume watano kuishia njiani na kubaki wawili ambao hadi leo wapo katika kikundi hicho wakishirikiana na wanawake kwenye kukuza mapato ya kikundi.
“Kwa kuwa mradi wetu ulikuwa ni wa kuimba, wanaume waliojiunga katika kikundi walijiondoa wakisema kuwa wanachekwa na washikaji zao kuwa wanaimba kama akina mama. Lakini sisi hatukukata tamaa, tuliendelea,” amesema.
Amesema baada ya muda waliamua kujikita katika shughuli za utunzaji wa mazingira kwa kuokota mbegu za miti, kupanda miche ya miti na kuiuza kijijini na vijiji vya jirani na wilaya hiyo.
Kudra amesema baada ya muda mfupi, walipata ufadhili kutoka Shirika la Uhifadhi Wanyamapori Afrika (AWF) ambalo lilinunua miche 35,000 kwa bei ya Sh400 kila mmoja huku wanakijiji wakichangia Sh100.
Kudra amesema baada ya mradi huo, waliamua kununua kiwanja na kujenga ofisi yenye thamani ya Sh57 milioni ili kuachana na kutumia nyumba za wanachama ambazo wakati mwingine ziliwafanya washindwe kufanya vikao wanapokuwa wenye nyumba hawapo.
Amesema mafunzo waliyoyapata kupitia mradi wa Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (O&OD), unaoendeshwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Nchini Japan (Jica), umewawezesha kugeuza vikwazo kuwa fursa.
Amesema walianzisha mradi mwingine wa ufugaji nyuki ambapo hivi sasa wana mizinga 57.
“Kwa kweli baada ya kuanza kugawana faida inayotokana miradi tuliyonayo, sasa wanakikundi wamepata nyumba bora na mapenzi ndani ya nyumba yameongezeka, wanaume hawawezi tena kutuolea wanawake wengine,” amesema.
Amesema awali walikuwa na maisha mabaya, walikuwa wakilalia vitanda vya kamba lakini sasa wanakikundi wamenunua magodoro na vitanda.
“Chumvi ikiisha unaenda kununua, humuulizi tena baba, ugolikipa kwa wanawake umeisha. Na fedha nyingine tumeziweka benki baada ya kufungua akaunti,” amesema Kudra.
Amesema awali wakati wakishinda mashambani kupanda miche ya miti, baadhi ya wanaume walikuwa wanasema,
Tunakwenda kushinda huko mashambani kwa kuwa tunawafuga wame zetu.”
Amesema hata hivyo hivi sasa maneno hayo hayapo tena kwa kuwa wameondoa chuki inayotokana na wao kutegemewa kwa kila kitu.
Kudra amesema kupitia kikundi hicho ameweza kupata fedha za kuwasomesha watoto wake wa kike ambao hivi sasa mmoja ni mwanajeshi na mwingine ni mtendaji (bila kutaja wanapofanyia kazi).
Kwa upande wake, mwanachama wa kikundi hicho, Sophia Momba amesema elimu waliyoipata katika kikundi imewasaidia kuongeza ujasiri, kwani zamani mke wa mtu ukijishughulisha na vikundi vya uzalishaji ama uelimishaji ulikuwa unaonekana kama umeshindikana.
“Hata katika masuala ya elimu mtoto wa kiume ndiye aliyekuwa akipewa kipaumbele, hawa kike walikuwa wanaonekana hawastahili lakini hivi sasa hali imebadilika wote wanapata elimu kwa usawa,” amesema Sophia.
Naye Stella James amesema kutokana na mafanikio ya kikundi hicho, wamegawana fedha kati ya Sh500,000 hadi Sh800,000 kulingana na kiasi kinachopatikana kwenye miradi ya utunzaji wa mazingira, uelimishaji wa jamii na ufugaji wa nyuki.
Mmoja wa wanaume kwenye kijiji hicho, Iddi Mnyika amesema uwepo wa kikundi hicho umechangia katika kuzuia ukatili kwa wanawake baada ya kujiwezesha kimapato.
“Hata ule mpango wa wanawake kuzururazura mtaani hakuna tena. Kipindi cha nyuma wanawake walikuwa wamedharaulika sana kutokana na familia walizokuwa wanaishi, mabinti walikuwa wao ni watu wa nyumbani, hawasomi kama ilivyo hivi sasa,” amesema.
Naye Mwakilishi Mkuu Ofisi ya Jica, Ara Hitoshi amesema mfumo wa O&OD ulianzishwa nchini mwaka 2001 ingawa mwaka huu unatimiza miaka 70 tangu uanzishwe katika nchi nyingine.
Amesema mfumo huo una lengo la kuhamasisha juhudi binafsi kwa wananchi na ushirikiano wa Serikali na jamii.
“Mfumo ulianzishwa kuhimiza mipango shirikishi ya maendeleo ya ndani. Mradi ulitoa mafunzo ya vitendo kwa maofisa ugani na kuwa wawasilishaji wa kata,” amesema.