Yafahamu anayopitia mtoto asiyemjua baba

Majuzi nilikutana na Salome (si jina lake halisi) akinielezea masikitiko yake ya kutokumfahamu baba yake. Salome (23), mwanafunzi wa chuo kikuu, ana maumivu makali ya kutafuta kumfahamu baba yake kwa miaka mingi bila mafanikio.

Nilitaka kuyaelewa vizuri maumivu yake. Salome anaeleza, “Najiona kama mtu mwenye bahati mbaya sana maishani. Ninajisikia kupungukiwa kitu cha muhimu kwenye maisha yangu. Kuishi bila kumfahamu baba yangu ni pigo kubwa na linanitesa na kuniumiza.”

Je, Salome amefanya juhudi gani kumfahamu baba yake?

“Nimeongea na mama mara nyingi kuhusu hili na hakunipa majibu yanayoeleweka. Mwanzoni nikiwa mdogo aliniambia baba yangu alifariki nikiwa mchanga bado. Baadaye nilikuja kubaini alinidanganya.

“Siku moja (miaka mitano iliyopita) nilisikia mazungumzo yake na bibi (ambaye ni mama yake) kuwa angetamani siku anakufa asikie ugomvi wa mama yangu na mume wake (baba yangu) uwe umeisha.” Salome anasema wakati huo bibi alikuwa mgonjwa sana na ilikuwa kama anaacha wosia kwa mama yake. Wote wawili hawakujua alikuwa anasikia mazungumzo yao.

“Siku hiyo sikulala usingizi. Nilifikiri mambo mengi yaliyoniumiza sana. Kwa nini nimefichwa baba yangu? Sikuwa na ujasiri wa kumwambia bibi wala mama, lakini angalau nikawa nimefahamu kuwa baba yangu yupo. Kuanzia wakati huo nilianza rasmi kufuatilia taarifa za baba yangu alipo. Niliuliza ndugu wengi ninaowafahamu na halikuwa jambo rahisi kumfahamu baba yangu.”

Salome bado hajafanikiwa kukutana na baba yake. Hata hivyo, amefahamu kuwa wakati anazaliwa palikuwa na mgogoro mkubwa kati ya mama na baba yake. Mgogoro huo ulimfanya aamue kumuondoa baba yake katika historia ya maisha yake.

Tunajua watu wengi tu wameishi bila baba na maisha yanaendelea. Wengine wamefiwa na baba zao, wengine wamegombana nao na hivyo hawataki mawasiliano ya aina yoyote. Kipi ni tofauti kwa Salome asiyejua baba yake ni nani?

 Tunazungumza na Salome kufahamu mengi zaidi. Salome anazungumza kwa uchungu mkubwa. “Najua kuna ile unajua baba yako ni marehemu au basi hujawahi kumwona, lakini unajua ametoka kwenye ukoo upi unaoweza kujitambulisha nao. Ukitaka kuelewa uchungu wangu fikiria unapotafakari historia yako inakuwa kama inatazama filamu inayokatika katika na unashindwa kuunganisha baadhi ya vipande. Inaumiza sana.

“Kuna wakati najiona kama mtu asiyekamilika, asiyejulikana vizuri ametokea wapi. Najiona nimepungukiwa kitu. Najiona kama bado sijielewi vizuri kama watu wengine. Ni sawa na mtu anayejua ana mkono wake mahali lakini anaishi bila mkono huo.”

Maisha yake yamekuwaje bila baba?

Salome anafuta uso wake kwa viganja vyake. Lindi la majonzi halifichiki. “Kuna wakati natamani niwe na mwanamume ninayemwamini na ninayejua hawezi kuwa na malengo mengine na mimi ninayeweza kumwambia mambo yangu ya ndani akanisikiliza kama mwanaye. Kuna mambo mengi nayatazama kwa jicho lililopungua na naamini baba yangu angenisaidia kuyatazama kwa upana zaidi.”

Kisaikolojia, sauti ya baba ni muhimu kwenye maisha ya mtoto. Ingawa miaka ya mwanzo ya mtoto mama ndiye anayehitajika zaidi kumhakikishia mtoto msalama wake, kuanzia miaka mitatu na kuendelea, mtoto huhitaji zaidi sauti ya mamlaka ya baba.

Baba huleta msawazo mzuri kimalezi unaopandikiza vizuri zaidi dhana ya mamlaka ya mzazi kwenye maisha. Baba, kadhalika, ndiye anayebeba jukumu la kumfanya mtoto aone matokeo ya tabia zake na kuthibitisha kile anachojifunza kwingineko.

Ingawa kazi hii inaweza kufanywa na mama, changamoto ni uwezekano wa kumchanganya mtoto anayeamini kuwa mama ndiye usalama wake wa kisaikolojia.

 Bruce D Perry, gwiji wa sayansi ya tabia, mwandishi mwenza wa kitabu cha “What happened to you? Conversations on Trauma, Resilience and Healing,” analieleza hili kwa lugha rahisi: “Mama ni faraja ya mtoto. Tunamtegemea mama kutufanya tujisikie salama na hilo linatupa ujasiri kama watoto. Mama anapogeuka kuwa mamlaka inayoadhibu na kuonya mara kwa mara mtoto anaweza kuchanganyikiwa. Mtu ambaye niliamini ndiye usalama wangu anapogeuka na kuwa mbwekaji, mkorofi anayenisema muda wote hilo linaweza kuleta tahayaruki.”

Perry anaendelea, “Hakuna mtu huwa anawafundisha wazazi, lakini ukiangalia unaweza kuona namna baba anavyochukua nafasi yake kumwelekeza mtoto wakati mwingine kwa ukali na mama anabaki na wajibu wake wa kumjengea mtoto hali ya kujiona yuko salama.”

Hii inaweza kuwa moja ya sababu inayowafanya watoto wengi waendelee kuwa karibu zaidi na mama zao hata wanapokuwa watu wazima kuliko wanavyokuwa na baba zao. Baba alisimama kwenye nafasi ya kujenga mamlaka inayoelekeza na kuadhibu, wakati mama mara nyingi huchukua nafasi ya kuwa faraja ya mtoto.

Ingawa wapo akina mama wakali wanaoonekana kuchukua nafasi hii ya baba kimamlaka, bado tafiti huwa zinaonesha kuwa ukali huu wa mama unaongeza uwezekano wa changamoto nyingi za kitabia kwa watoto.

Msikilize Gordon Neufeld, mwanasaikolojia mahiri wa ki-Marekani, “Mtoto anapokosa mahali pa kukimbilia kwenye ngazi ya familia, unamwongezea uwezekano wa kuwa na tabia zitakazomsumbua baadaye. Usalama wetu uko kwa mama, ndiye huwa kimbilio kwa wengi wetu, lakini mamlaka yanayojenga hofu ya kukosea na kwenda kiyume na matarajio ya jamii inajengwa na baba.”

Sauti ya Baba katika malezi

Tafiti kadhaa zilizofanyika katika nchi zilizoendelea zinaonesha kuwa watoto waliokua bila baba wana nafasi mara dufu ya kuwa wakorofi, wababe na kujiingiza kwenye tabia za kihalifu ukilinganisha na wenzao waliolelewa na wazazi wote wawili.

 Hivi karibu Sara McLenahan na wenzake, kwa kutumia mbinu ya kufuatilia maendeleo ya watoto kwa muda mrefu, walibaini tofauti ya wazi kwenye eneo la afya ya akili.

 Sara, kwenye andiko lake, “The Causal Effects of Father Absence” anasema:

“Madhara ya kukosekana kwa baba kwenye maisha ya mtoto yamekuwa yakijadiliwa kwa ukosoaji mkubwa.

Wakosoaji wengi huhoji matumizi ya takwimu zisizowafuatilia watu kwa muda mrefu. Kwenye utafiti wetu tumetumia mbinu ya kuwafuatilia walengwa kwa muda mrefu.

Matokeo yanaonesha kuwa ukilelewa bila baba unakuwa na changamoto nyingi kwenye mahusiano yako na watu na namna unavyomudu hisia zako. Suala la afya ya akili linahusishwa kwa karibu sana na kukosekana kwa malezi ya baba kwenye maisha ya mtoto.”

Simulizi ya Salome inaweza kuwa mfano wa madhara haya yanayoelezwa na Sara McLenahan.

Sheria ya Mtoto Na 21 ya 2009 inatambua haki ya mtoto kuwa na utambulisho. Sura ya II ya sheria hiyo inayozungumzia haki na ustawi wa mtoto, kifungu cha 6(2) kinasema, “Mtu (yeyote) hatamnyima mtoto haki ya kuwa na jina, utaifa na kuwafahamu wazazi wake waliomzaa na ndugu wengine wa familia tandaa kwa kutegemea matakwa ya sheria nyingine zilizoandikwa (tafsiri isiyo rasmi).”

Sheria hii inazingatia ukweli kuwa utambulisho wa mtu haukamiliki bila kuelewa mizizi yake ya kifamilia. Mtu asiyemfahamu baba yake, kwa mukhtadha huu, anakuwa na utambulisho nusu nusu unaoweza kumpa usumbufu mwingi wa kisaikolojia.

Ingawa sheria inawataka wazazi kumpa mtoto haki hiyo, baadhi ya wazazi, wakiwemo wazazi wa Salome, kwa sababu mbalimbali huwanyima watoto haki hiyo ya msingi.

 Kwa mujibu wa sheria hii, uamuzi wa mtu kumficha mtoto baba yake ni kosa.

Utatuzi chanya wa migogoro

Tunatambua, kwa hakika, yapo mengi yanayoweza kuvuruga mahusiano ya wapenzi wawili kiasi cha mmoja kuona suluhu ya uhakika ni kumuadhibu mtoto kwa kumnyima haki ya kumjua mzazi wake.

Kwa mfano, yanaweza kuwepo mazingira ambayo baba anakuwa tatizo la kwelikweli linalozorotesha afya ya akili ya mwanamke aliyezaa naye. Katika hali kama hii, ni rahisi mwanamke kuamua kumtumia mtoto kama silaha ya kupambana na matatizo yake ya kimapenzi.

Ingawa uamuzi kama huu unaweza kuonekana ni sawa kwa haraka, lakini madhara yake yanaweza kuwa makubwa kwa mtoto kama tulivyokwisha kuona. Kwa nini tutengeneze mduara wa athari mbaya kwa jamii kwa kutokujifunza namna bora ya kutatua changamoto zetu bila kumnyima mtoto haki ya kuwa na utambulisho uliokamilika?

Pamoja na hasira, uchungu na kisasi, bado tunaweza kutafuta namna chanya ya kuponya nafsi zetu bila kuwanyima watoto haki yao ya msingi ya kuhusiana na baba zao kama anavyoeleza Dafroza Hemedi (35) mkazi wa Dodoma,

“Niligombana sana na mwanaume niliyezaa naye mtoto wangu wa pekee. Nilishindwa kabisa kuishi na ukatili uliopitiliza alionifanyia kwa muda mrefu nikiwa mjamzito. Ukiacha kunifanya nikose elimu kwa kukatisha masomo wakati huo, wazazi wangu walinikataa na kunifukuza.”

 “Hatukumaliza tofauti zetu mpaka sasa. Lakini namshukuru Mungu nilipata msaada wa kuelewa umuhimu wa mtoto kumfahamu baba yake. Ilikuwa ngumu sana, lakini nilifanya uamuzi mgumu wa kulinda haki ya mwanangu kuwa na baba yake mzazi.”

Dafroza bado ana mgogoro mkubwa na baba wa mwanaye. Hawazungumzi wala kusalimiana. Hata hivyo, mtoto wake ana uhusiano mzuri na baba yake.

“Huwa natamani nimuadhibu mwanamume yule kwa kumnyima mtoto. Nina kisasi kikali sana kwa mengi aliyonifanyia. Lakini natambua kuwa ninaweza kuwa na njia nyingine ya kupambana na mwanamume huyu bila kuathiri hitaji la mwanangu kumfahamu baba yake.

 Ingawa ni kweli tunaweza kuumizwa na wazazi wenzetu, ni muhimu kukumbushana kuwa matatizo yetu sisi watu wazima yanaweza kuharibu kabisa utoto wa watoto wetu. Tunaweza kutunza utoto wa watoto wetu kwa kuwaepusha na migogoro ya kiutu uzima isiyowahusu.

Related Posts