Moshi. Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, Ludovick Joseph Minde amewataka wasomi nchini kutumia elimu walizozipata kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka vitendo vya wizi na ubadhirifu katika nafasi mbalimbali walizopewa kulitumikia Taifa.
Askofu Minde ametoa rai hiyo Jumamosi ya Septemba 28, 2024 kwenye maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya miaka 25 ya shule ya St. Mary Goreti, yaliyofanyika shuleni hapo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amesema wizi na ubadhirifu kwa sasa umezidi katika taasisi mbalimbali za Serikali na hata za kanisa na kueleza kuwa ni lazima wasomi hasa wale waliosoma katika shule za taasisi za dini kusimama imara na kuonyesha hofu ya Mungu katika utendaji kazi wao.
“Wizi umezidi katika taasisi mbalimbali za nchi yetu za Serikali na hata za kanisa, sasa watu kama nyinyi (wasomi) lazima mkaokoe hali inayoendelea vibaya, watu wajue watu hawa kweli ni wenye hofu ya Mungu na wamefundishwa maadili, waone kama watumishi waaminifu na wanamuangalia Mungu kama kioo chao cha kazi,” amesema.
Amesema katika shule za taasisi za dini, wanafunzi wamekuwa wakifundishwa maadili mema, unyenyekevu na uadilifu, hivyo ni vyema wakayaishi maisha hayo hata watakapopata kazi na kuwa watumishi katika taasisi mbalimbali.
Akizungumzia shule ya St. Mary Goreti, Askofu Minde amesema imekuwa chachu katika kutoa wanafunzi wenye nidhamu na uadilifu, hivyo amewataka kuendeleza uaminifu huo hata watakapopata kazi na kuhakikisha wanakuwa mfano wa kuigwa katika jamii.
“Wewe kama mfanyakazi uliyesoma shule ya St. Mary Goreti mahali popote mtakapokuwa, mkawe watu wenye hofu ya Mungu, muache uovu, muache kutenda matendo ya ajabu ajabu, maana mmelelewa katika misingi ya kumjua Mungu.
“Mnapokuwa katikati ya watu, mkawe watendaji, watumishi watendaji, waaminifu na wachapa kazi ili mfanikiwe, ukiwekwa benki usichukue hata senti moja, usiibe chochote, wewe uliyesoma hapa, umefundishwa vizuri mkaishi maisha ya Yesu,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Wilson Mahera amesema shule hiyo imetoa funzo kwa shule na taasisi nyingine kuhakikisha zinakuwa na uongozi mzuri, ili kuchochea chachu ya ukuaji wa taaluma.
“Shule hii inaonyesha ina uongozi mzuri, kwani kuna walimu na wafanyakazi wako hapa kwa miaka 25 tangu ianzishwe, nadhani kuna haja ya shule zetu kujifunza hapa, kwani ukiona watu wamekaa mahali muda mrefu, ujue uongozi ni mzuri na unachangia matokeo kuwa mazuri au kuwa mabaya.
“Hongereni kwa kuweka msingi mzuri na malezi bora kwa vijana wetu, suala la nidhamu ni muhimu sana, tuna changamoto kubwa lakini walimu mtusaidie kuhakikisha watoto wanabaki kwenye maadili mema na wanafunzi watambue siri pekee ya mafanikio ni nidhamu, kujituma, kufanya kazi kwa bidii na kujitambua,” amesema.
Dk Mahera ametumia pia nafasi hiyo kuwataka wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata chakula cha mchana shuleni, ili kuchochea ukuaji wa taaluma.
“Rais amewekeza katika sekta ya elimu na sasa tuna mkakati wa kujenga shule za amali katika kila mkoa na fedha zipo, lakini pamoja na Serikali kuwekeza kwenye majengo, walimu na kwingine Nanyi wazazi tambueni ni wajibu wenu kuhakikisha watoto wanapata chakula cha mchana shuleni na hii itamfanya kuwa na akili nzuri,” amesema.
Mkuu wa shule hiyo, Sista Clementina Kachweka amesema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1999 ikiwa na wanafunzi 120 na walimu saba na kwamba tangu kuanzishwa kwake miaka 25 iliyopita, wanafunzi 6,984 wamehitimu, wakiwamo wa kike ni 6,233 na wa kiume 751.
Amesema kwa sasa shule ina jumla ya wanafunzi 1,000, ambapo kati ya hao, wa kike ni 759 na wa kiume ni 241 na wanafunzi wote wa kike wanaishi katika hosteli ya shule.
Sista Kachweka amesema wazo la kuanzishwa kwa shule hiyo ni uhitaji wa elimu kwa kundi la watoto wa kike ambao walikuwa na nafasi finyu kielimu na kwamba moja ya malengo yalikuwa kumkomboa mtoto wa kike katika nyanja zote.
Kwa mujibu wa mtawa huyo, malengo mengine yalikuwa ni kumjenga Mtanzania ambaye amefungamana na mzalendo na kumuandaa raia ambaye yupo tayari kuwatumikia raia wenzake kwa upole, upendo na weledi mkubwa.