KIUNGO wa Simba, Awesu Awesu amefunguka siri ya ushindi wa timu yake dhidi ya Dodoma Jiji kuwa ni kufanyia kazi maagizo aliyopewa na kocha wa timu hiyo Fadlu Davids.
Ipo hivi; Awesu aliingia kipindi cha pili dhidi ya Dodoma Jiji baada ya Simba kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza bila ya kufungana na wapinzani wake na baada ya kuingia anaeleza kuwa kocha alimsisitiza kutoa pasi za haraka bila ya kukaa na mpira.
“Kocha aliniambia sitakiwi kukokota mpira nikiwa eneo la goli la wapinzani wetu zaidi nipushi mashambulizi kwa uharaka hicho ndio nilichokifanya na kusababisha madhara ndani ya 18 na timu kupata penalti,” amesema.
“Mchezo ulikuwa mgumu wapinzani walifanikiwa kuzuia njia zote ambazo kocha alikuwa anaamini ndio zitatoa matokeo hivyo mabadiliko yalitokana na namna ambavyo mwalimu aliwasoma wapinzani dakika 45 za kipindi cha kwanza.”
Awesu amesema hakuna timu rahisi hivyo wao kama wachezaji wanajiandaa kukabiliana na ugumu kutoka kwa mpinzani yeyote watakayekutana naye huku akisisitiza kuwa mipango mizuri ndio inawapa matokeo.
“Hakuna timu ambayo inaingia uwanjani ikiwa inafahamu kuwa inashinda au inafunga mipango mizuri baina ya wachezaji na benchi la ufundi ndio inaamua matokeo na ndio kilichotokea dhidi ya Dodoma Jiji,” amesema.
“Malengo yetu msimu huu ni kukusaya pointi kwenye kila mchezo bila kujali ni ugumu gani tutakutana nao na hilo linawezekana kwani kocha na sisi tuna mazungumzo mazuri na mipango thabiti, hivyo ubora ndani ya dakika 90 ndio utaamua.”
Simba imecheza mechi nne hadi sasa na imefanikiwa kukusanya pointi 12 baada ya ushindi kwenye mechi zote wamefunga mabao 10 kwenye mechi hizo wakianza na ushindi wa mabao manne dhidi ya Fountain Gate, mabao 3-0 Tabora United, 2-0 Azam FC na 1-0 Dodoma Jiji.