Kocha Mkuu wa Mashujaa, Mohamed Abdallah ‘Bares’ amesema alikiandaa kikosi chake kuvuna pointi tatu dhidi ya Azam FC, lakini moja waliyoipata ni uzembe wa washambuliaji.
Mashujaa imecheza mechi tano ikishinda mbili dhidi ya Dodoma Jiji kwa bao 1-0, Coastal Union 1-0, sare tatu dhidi ya Azam, Tanzania Prisons 0-0 na Pamba Jiji 2-2.
Amesema mchezo ulikuwa mzuri kwa pande zote, lakini umakini mdogo wa washambuliaji ndio uliwakwamisha kukusanya pointi tatu kwenye uwanja wa nyumbani huku akiwamwagia sifa mabeki wa timu hiyo.
“Maandalizi yetu yalikwenda vizuri tulikutana na mpinzani ambaye tulimfanyia tathimini nzuri kabla ya kuvaana naye, nawapongeza wachezaji wangu kwakuwa walifanya kile nilichowaelekeza waliniangusha kwenye umaliziaji,” amesema na kuongeza.
“Walinzi walifanya kazi sahihi kuondoa hatari zote zilizokuwa zinaelekezwa langoni kwetu mpango huu ukiendelea hadi kwenye mechi zilizosalia tutakuwa na timu bora yenye ushindani.”
Kwa upande wa beki wa timu hiyo, Omary Kindamba amesema licha ya kuruhusu mabao mawili kwenye mechi tano bado wana kazi ya ziada kuhakikisha hawarudii makosa.
“Kama mabeki tunajisikia vibaya kuruhusu mabao na hatukutakiwa kuruhusu lakini kwa hapa tulipo tunakwenda vizuri nafikiri tunahitaji muendelezo tu,” amesema na kuongeza:
“Mechi ijayo tunacheza na Singida Black Stars wameanza vizuri ligi na ni miongoni mwa timu bora kwa sasa ingawa kwa matokeo hatutofautiani sana.”
Oktoba 2, Mashujaa itaikaribisha Singida Black Stars ambayo iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imekusanya pointi 13 na mara ya mwisho timu hizo kukutana Wazee wa Mapigo na Mwendo waliichakaza timu hiyo kwa mabao 2-0.