Jina Dar es Salaam, ni neno lenye asili ya Kiarabu ‘Daarul Salaam’ yaani nyumba ya amani.
Kwa mujibu wa historia iliyomo kwenye wavuti wa mkoa, Jiji la Dar es Salaam linaelezwa kuanza kama kijiji kidogo cha wavuvi kilichojulikana kama Mzizima yaani mji wenye neema au afya.
Japo mji unatajwa zaidi kuanza miaka ya 1850, lakini kuna historia inayoonyesha kuwa eneo hilo lina historia ya miaka 1000 iliyopita likiwa limekaliwa na wavuvi hao wajulikanao kwa jina la Wabalawa waliochanganyika na Wazaramo.
Inaelezwa kuwa Wabalawa na Wazaramo hawa walikuwa wakiishi maeneo kama Mbwa Maji (Kivukoni), Geza Ulole na Mji Mwema.
Taswira halisi ya mji hata hivyo haikuonekana mpaka ulipokuja ujio wa Masultan (Waarabu) kutoka Zanzibar na baadaye Wajerumani na kisha Waingereza.
Wavuti wa mkoa unaeleza kuwa ujenzi wa makao ya Sultani Majid bin Said kutoka Zanzibar pamoja na bandari, ulianza rasmi mwaka 1865 katika eneo la kijiji hicho. Ni Sultan huyo aliyeupa mji huu jina la Daarul Salaam akimaanisha nyumba ya amani au unaweza pia kuita bandari ya salama.
Ujenzi wa makao makuu ya Sultan ulikamilika mwaka 1866 na Sultan akahamia eneo hilo kitendo kilichofanya eneo hilo kutanuka na uchumi wake kukua kwa kasi kubwa japo kwa kipindi kifupi ambapo Sultani Majid bin Said aliishi.
Alipofariki mwaka 1870, kifo chake kilisababisha kudidimia kwa maendeleo ya mji wa Dar es Salaam, kabla ya hali hiyo kubadilika mwaka 1884 kufuatia kuanzishwa kwa koloni la Wajerumani la Afrika Mashariki.
Ukiwa na kilomita za mraba 1,800, Mkoa wa Dar es Salaam, ulianzishwa kutoka Mkoa wa Pwani mwaka 1973 ukiwa na wilaya tatu amabazo ni Ilala, Kinondoni na Temeke