Familia ya Sokoine: Imetuchukua miaka 40 ndoto ya kuandika kitabu cha mzee kutimia

Dar es Salaam. Familia ya hayati Edward Moringe Sokoine imeelezea panda shuka ya safari ya miaka 40 katika kutimiza ndoto yake ya kuweka maisha ya kiongozi huyo katika maandishi.

Mtoto wa marehemu, Balozi Joseph Sokoine ameeleza namna familia ilivyojitahidi kufanikisha hilo kwa miaka kadhaa, kabla ya Machi 2021 kupokea simu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, ikiwataka kuwasilisha taarifa walizonazo kuhusu hayati Sokoine.

Balozi Sokoine amesema hayo leo Jumatatu Septemba 30, 2024 katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha Edward Moringe Sokoine (Maisha na Uongozi Wake), hafla ambayo imehudhuriwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Edward Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa tatu wa Tanzania. Alikuwa Waziri Mkuu mara mbili, tangu Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980  na mara ya pili kuanzia Februari 24, 1983 hadi Aprili 12, 1984 alipofariki dunia kwa ajali ya gari.

Ajali hiyo ya gari ilitokea eneo la Wami-Dakaya, Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro akiwa njiani kurejea jijini Dar es Salaam akitokea mjini Dodoma alikokuwa akishiriki vikao vya Bunge.

Katika maelezo yake, Balozi Sokoine amesema: “Miaka 40 ya kusoma kitabu cha maisha na mmoja wa viongozi wa Tanzania imetimia kwa msaada wako Rais Samia Suluhu Hassan. Nakumbuka Machi 2021 nilipokea simu kutoka kwa msaidizi wa Makamu wa Rais akihitaji kupitia taarifa za mzee.

“Nilimweleza nina kitabu cha hotuba aliyoitoa Machi 1983 na nikamweleza kuna hotuba nyingine aliyoitoa Oktoba 1982 kwenye mkutano mkuu wa chama na kwamba hotuba nyingine za mzee zinaweza kupatikana kwenye hansadi, nilimuahidi kumtumia kitabu hicho na nilifanya hivyo,” amesimulia.

Balozi Sokoine amesema baada ya muda mfupi alipokea simu nyingine kutoka Makamu wa Rais akiuliza kama kuna kitu kingine cha ziada ambacho Sokoine aliandika, “Nikamweleza kipo pia kitabu cha mwaka 1984 na 1985 kilichoeleza juu ya maisha ya mzee kidogo na hotuba zake na hakikuwa na uchambuzi wa kina.

“Nilimweleza juhudi za familia kwa zaidi ya miaka 30 ya kutaka kuandika kitabu, baada ya maelezo yale alinieleza kuhusu umuhimu wa kuandika kitabu cha watu mashuhuri, ili tusipoteze urithi na sehemu ya historia ya nchi yetu. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliniambia nimwachie suala hilo na ataona cha kufanya atawasilisha na kwamba angeliwasilisha kwako Rais,” amesema.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na mtoto wa hayati Edward Sokoine, Balozi Joseph Sokoine kabla ya kuzindua kitabu kinachohusu maisha na uongozi wake katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) leo Septemba 30, 2024.

Balozi Sokoine ameongeza baada ya mazungumzo hayo, Makamu wa Rais, Dk Mpango alifikisha jambo hilo kwa Rais Samia Suluhu Hassan na muda mfupi alilitolea maelekezo kwamba Uongozi Institute watakuwa waratibu wa kitabu hicho pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).

“Familia tulifurahi kwamba matamanio yetu ya miaka mingi yanakwenda kufanikiwa, tunakushkuru sana Rais Samia, hatuna cha kukupa zaidi ya kukupa asante sana na Mungu akuongoze.

“Shukrani pia kwa Makamu wa Rais kufikisha ujumbe wetu kwa Rais, ulisimamia hatua kwa hatua, uandishi wa kitabu na tunazidi kukuombea kwa Mwenyezi Mungu,” amesema Balozi Sokoine.

Amesema pamoja na kuwa ni miaka mingi imepita na wengi ambao wangeweza kuelezea hawapo duniani, familia ilishawahi kupewa angalizo kuhusu uandishi wa kitabu hicho.

“Nakumbuka rafiki yangu alisema kila kitu kinatokea kwa mipango ya Mungu na hiki kimeandikwa na kutoka baada ya mipango ya Mungu.”

Amesema familia ya Sokoine ilianza na mchakato wa uandishi wa kitabu hicho tangu Serikali ya awamu ya kwanza chini ya utawala wa Mwalimu Julius Nyerere.

“Balozi Ombeni Sefue tumewahi kuzungumza kuhusu kitabu hiki, kimekuja kukamilika wakati wa uongozi wako awamu ya sita na Mungu alikuwa na maono yake kifanyike wakati huu,” amesema.

Pamoja na hayo, Balozi Sokoine amewashkuru viongozi mbalimbali wa kitaifa kutoka Bara na Visiwani waliowahi kufanya kazi na hayati Sokoine waliokutana na waandishi na kukubali kufanya mahojiano na kutoa ushirikiano.

Amesema kitabu hicho ni urithi wa kizazi cha sasa na baadaye na kwamba walizingatia tahadhari zote walizopewa kuhusu uchapishaji wa kitabu hicho.

“Kiongozi mmoja alitupa tahadhari kwamba kuandika kitabu hiki si kazi rahisi, kama ikiwa taarifa zitapotoshwa kumhusu mzee na yeye hayupo hawezi kuelezea kuhusu kitabu hiki.

“Waandishi wamekwenda mikoani na maeneo mbalimbali kukusanya taarifa na tunawashkuru waliokihariri pamoja na Mkuki na Nyota wachapishaji wa kitabu hiki. Tumeiachia nchi hazina ya kiitabu hiki,” amesema Balozi Sokoine.

Kitabu hicho kimeandaliwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Uongozi na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), kinaangazia safari yake, kuanzia makuzi yake katika jamii ya kimasai hadi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi, ikiwemo uwaziri mkuu wa Tanzania. Pia kitachangia kukuza historia ya Tanzania na Bara la Afrika.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi

Related Posts