Hadhara anahitaji msaada, amlilia Samia

MKALI wa kucheza danadana, Hadhara Charles, hali yake si nzuri kama alivyozungumza na Mwanaspoti katika mahojiano gazeti la juzi Jumamosi, huku mwenyewe akikiri wakati mwingine umaarufu alionao umekuwa kama mzigo kwake.

Hadhara ambaye alijipatia umaarufu kutokana na uwezo wake wa kuchezea mpira kwa ustadi mkubwa kwa kutumia viungo mbalimbali vya mwili, licha ya kujulikana anajikuta ana maisha magumu na sasa anamwomba Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan asikie kilio chake.

Alisema kuna wakati akipita barabarani, inakuwa ngumu kusaidika, kwani wengi wanamuona amesafiri nchi mbalimbali, anawezaje kuishi maisha duni kiasi kile.

“Hakuna kazi inayokosa changamoto, mfano wanawake baadhi ndio waliokuwa wananicheka mtaani, wakati nafanya kazi ya kuchezea mpira na waliona kama nina kichaa, lakini nilikuwa napata pesa ya kula na watoto wangu,” alisema Hadhara anayesumbuliwa na maradhi ya kupoteza fahamu na miguu, kiasi cha kushindwa kuifanya kazi yake kwa ufanisi tofauti na siku za nyuma.

“Unajua watu wakikuona unapanda ndege, umepiga picha na watu maarufu ama viongozi wanaona una pesa, sina kitu, ndio maana naamini kupitia gazeti la Mwanaspoti naweza nikasaidika watu wakiniona maisha yangu halisi, tofauti na ukubwa wa jina langu lilivyo mitandaoni,” alisisitiza.

Kilio chake alikipeleka kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ili baadhi ya mikutano yake, amwalike akaonyesha kipaji chake, aweze kujipatia pesa ya kujikimu kimaisha.

“Naomba wanipe kazi ndipo nipate pesa, namwomba Rais wetu, mama yangu Samia Suluhu, nikionyesha shoo katika mikutano yake, nitapata kitu chochote cha kuendesha maisha yangu,” alisema Hadhara na kuongeza;

“Natamani watu wamwonyesha Rais Samia video zangu, aone ninachokifanya, mimi niliiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Afrika ya kuchezea mipira, nilikuwa namba tatu, ni mwanamke ninayepambana, najua yeye ni muumini wa kusapoti michezo.”

Hadhara anayesumbuliwa na ugonjwa wa kupoteza fahamu, anasema anatamani angepata msaada angetibiwa na ikiwezekana kufanya biashara zake, ili maisha mengine yaendelee.

“Ukiachana na ugonjwa wa kupoteza fahamu, ninasumbuliwa na miguu, nikipata pesa najua naweza nikapata matibabu,” alisema Hadhara mjane mwenye watoto wawili.

Kwa yeyote ambaye angependa kumsaidia mwanadada huyo anaweza kumtumia kupitia pesa kupitia TigoPesa namba 0717-171386 muamala utasoma jina la HADHAR ABDU.

Related Posts