KILUPI : AWATAKA VIONGOZI WA DINI KUKEMEA UKABILA

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Omar Ibrahim Kilupi amewasihi viongozi wa dini mbalimbali nchini kukemea tabia za baadhi ya wanasiasa waohamasisha siasa za udini,ukanda na ukabila.

Kauli hiyo ameitoa wakati akiwahutubia waumini wa dini ya kikiristo katika hafla ya kutimiza miaka 30 ya Kwaya Mtakatifu Michael Malaika Mkuu Parokia ya Mpendae Zanzibar.

Kilupi, amesema viongozi wa dini nchini wanatakiwa kuelekeza nguvu zao katika kuhubiri na kutoa mafundisho ya kiimani ya kukemea kauli za uchochezi na ukabila zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa kwani zinaweza kuingiza nchi katika machafuko.

Alieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi,wameasisi maridhiano ya kisiasa na kuruhusu utawala wa kidekrasia hivyo ni muhimu kwa kila mwananchi kuheshimu misingi hiyo.

Alisema kuna baadhi ya wanasiasa na wanahatakati wameanza kutoa kauli zinazoashiria uvunjifu wa sheria tabia zinazotakiwa kupingwa na wananchi wote bila kujali tofauti zao za kisiasa na kidini.

Katibu huyo Kilupi, aliwasihi viongozi na waumini hao kuendeleza umoja,mshikamano na upendo wakati wote sambamba na kuiombea nchi iendelee kuwa na amani na utulivu.

“Wito wangu kwenu endeleeni kuwa wamoja msikubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa wanaohamasisha vurugu na kauli za kuwabeza viongozi wetu wakuu wa kitaifa kwani maendeleo yanayotekelzwa nyote mnayaona.

Amani ndio chimbuko la maendeleo haya tuliokuwa nayo hivi sasa hivyo tusikubali fursa hii ituponyoke kwa gharama yoyote.”,alisema Kilupi.

Kupitia sherehe hiyo, alisema CCM imeendelea kusimamia sera zake kwa kuhakikisha serikali inatekeleza kikamilifu maendeleo kama ilivyoahidi katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Pamoja na hayo aliwasisitiza waumini hao kutumia vizuri haki yao ya kidemokrasia kuhakikisha wanajiandikisha katika awamu ya pili ya daftari la kudumu la wapiga kura ili wapate uhalali wa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Naye Padri Antony Kanturu wa Kanisa Katoriki la Mtakatifu Michael Malaika Mkuu Parokia ya Mpendae Zanzibar alisema kipaumbele cha kanisa hilo ni kutoa mahubiri yanayowaunganisha wananchi katika kuendeleza amani na upendo.

Katika risala ya Kwaya hiyo walisema kwa kipindi cha miaka 30 wamepata mafanikio mbalimbali yakiwemo kurekodi na kutengeneza albamu za nyimbo mbalimbali zinazoendelea kufanya vizuri katika soko la nyimbo za kwaya ndani na nje ya nchi.

Kupitia risala hiyo walitaka changamoto zinazowakabili ni ukosefu wa gari ya kutoa huduma za usafiri pamoja na ukosefu wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya uandaaji wa nyimbo.

Kwaya hiyo ya Mtakatifu Michael Malaika mkuu ya Kanisa Katoriki Parokia ya Mpendae ilianzishwa mwaka 1994 ikiwa na idadi ya wanakwaya 15.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Omar Ibrahim Kilupi,akiwa na Viongozi wandamizi wa Kanisa Katoriki Parokia ya Mpendae Zanzibar, katika sherehe ya kutimiza miaka 30 ya Kwaya ya Mtakatifu Michael Malaika Mkuu ya Kanisa Katoriki Parokia ya Mpendae Zanzibar.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Omar Ibrahim Kilupi, akizungumza katika sherehe ya kutimiza miaka 30 ya Kwaya ya Mtakatifu Michael Malaika Mkuu ya Kanisa Katoriki Parokia ya Mpendae Zanzibar.

Related Posts