MALAWI ndio pekee iliyotoa upinzani mkali kwa Tanzania katika mbio za kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa kriketi ya mizunguko 20 ambapo Tanzania ilishinda kwa mikimbio 19 tu katika mchezo wake wa hitimisho.
Kwa Tanzania ilikuwa ni jambo linalotegemewa kushinda michezo yote mitano, lakini haikuwa rahisi mbele ya Malawi ambayo michuano hii imewapa tija kubwa ikiwamo kufuzu fainali za Kombe la Dunia kama washindi wa pili nyuma ya Tanzania.
Licha ya kuwa ni mchezo wa nchi zinazoongea Kiingereza, hapo awali Malawi haijawahi kuwa bora katika kriketi kama ilivyo Kenya, Uganda, Zimbabwe, Afrika Kusini, Tanzania na Botswana na mafanikio yao katika michuano ya Dar es Salaam ni ishara tosha kuwa mchezo huu umepiga hatua kubwa ya maendeleo nchini humo.
Katika mchezo huo ulipigwa mwishoni mwa juma kwenye Uwanja wa Dar es Salaam Gymkhana, Tanzania ndio iliyoshinda kura ya kuanza na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 119 baada ya wapigaji wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 19 kati ya 20 iliyowekwa.
Katika kujaribu kufukuzia mikimbio waliyoitengeneza Tanzania, Malawi walijitahidi sana lakini walijikuta wakigota na mikimbio 100 baada ya wote kutolewa wakiwa wametumia mizunguko yote 20 na hivyo kuifanya Tanzania kushinda kwa mikimbio 19 tu.
Mpigaji mwanzilishi wa Tanzania, Abhik Patwa alikuwa nyota wa mikimbio baada ya kupiga mikimbio 30 kutokana na mipira 27 akifuatiwa na Harsheed Chohan aliyeleta mikimbio 26 kutokana na mipira 11 na Kassimu Nassoro aliyetengeneza mikimbio 22 kutokana mipira 23.
Tanzania wakiwa mabingwa, Malawi walimaliza wa pili na kujiunga na Tanzania kucheza fainali.
Mtanzania Khalid Juma Amiri ndiye aliyetangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi ya fainali kati ya Tanzania na Malawi.
Ni dhahiri Malawi imefanya maendeleo makubwa katika kriketi kwani wachezaji wake wameweza kutawala upokeaji wa tuzo katika vitengo mbalimbali.
Mpigaji bora wa mipira (batsman) alikuwa ni Sami Sohail wa Malawi aliyetengenza jumla ya mikimbio 137.
Malawi pia ilitoa mrushaji (bowler) bora, Suhail Vayani aliyeangusha wiketi 13 za wapinzani na mlinda wiketi bora alikuwa Phillip Zuze pia wa Malawi aliyewatoa nje jumla ya wapigaji 10 wa timu pinzani.
Mchezaji bora wa vitengo vyote (all rounder) alikuwa ni Mghana Obed Harvey.