Mbeya. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Mbeya imesema inatarajia kukutana na vyama vyote vya siasa mkoani humo kuwakumbusha kuzingatia kanuni za uchaguzi, hasa kuepuka viashiria vya rushwa.
Uchaguzi wa serikali za mitaa umepangwa kufanyika Novemba 27, 2024 ili kupata viongozi wa ngazi za mitaa, vitongoji na vijiji kabla ya uchaguzi mkuu mwakani wa kuwapata madiwani, wabunge na Rais.
Akizungumza hivi karibuni katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mbeya, Maghela Ndimbo amesema ili kudhibiti vitendo vya rushwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi watakaa na vyama vyote kuwakumbusha.
Amesema mbali na majadiliano ya vyama hivyo, wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia kampeni yao ya ‘Takukuru Rafiki’ kuwaweka sawa kujiandaa na uchaguzi kwa kukwepa wagombea watakaotanguliza hongo ya namna yoyote na kuwafichua.
“Tunajua kila chama kina muongozo wake, hivyo sisi tunakwenda kuwakumbusha, wananchi nao tunaendelea kuwapa elimu kufichua wagombea au wapambe watakaoonyesha viashiria au kutoa rushwa,” amesema Ndimbo.
Ndimbo ameongeza kuwa kipindi cha uchaguzi huwa kunaibuka matukio mengi ya dalili za rushwa, ikiwamo wagombea, wapambe na wapigakura kutoa na kupokea rushwa zikiwamo nguo, vyakula, ajira na fedha, hivyo watakuwa makini kuwachukulia hatua watakaobainika.
Amesema mgombea atakayebainika, Takukuru itawasilisha ripoti kwa mamlaka za uchaguzi kumuengua, kwani atakuwa amekiuka sheria, kanuni na taratibu za nchi kikatiba.
“Kipindi cha uchaguzi ndio utaona nguo zinatolewa, vyakula, fedha, ajira na mengine. Rushwa inapaswa kukemewa na kupingwa na kila mmoja, hata kiongozi anayetoa rushwa ili achaguliwe hana sifa ya kuongoza” amesema kiongozi huyo.
Amesema kwa sasa wamejipanga kufanya mikutano ya mara kwa mara na kuwafikia wanafunzi wa vyuo vikuu ambapo mbali na kuhamasisha kujiandikisha na kupiga kura, watawapa elimu juu ya athari ya kuomba na kupokea rushwa.
Baadhi ya wananchi jijini hapa wamesema iwapo Takukuru itafanya kwa utekelezaji wa mpango huo, inaweza kusaidia uchaguzi kuwa wa huru na haki wakiomba watakaobainika kuwekwa wazi.
Ramadhan Msigwa, amesema Takukuru inapaswa kutenda haki kwa vyama vyote na watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote kwenye rushwa watangazwe na kuchukuliwa hatua.
“Wakati wa uchaguzi vitendo kama hivi lazima vitokee kwa kuwa baadhi ya wagombea wanaona kufanya hivyo ndio kuonyesha nia na utendaji wao, Takukuru isimamie sheria bila kubagua na itawakamata wengi” amesema Msigwa.
Kwa upande wake, Neema Gilla amesema wananchi nao wamekuwa sababu za kushawishi vitendo vya rushwa, wakiamini bila mgombea kutoa chochote hana sera wala hafai kuongoza, hivyo kuomba elimu kuwafikia wote.
“Kuwepo na elimu pia kwa wananchi wenyewe ambao ndio wapigakura, muda mwingine wao ndio wanatengeneza njia za rushwa, wakiona mgombea hatoi kitu wanaona hana uwezo wa kuongoza” amesema Neema.