MAAFISA WASAIDIZI WA UCHAGUZI HALMASHAURI YA WILAYA YA KIBAHA WAPATIWA MAFUNZO , WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA NA UADILIFU.

Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Bi. Regina L. Bieda, leo Septemba 30, 2024, ametoa mafunzo maalum kwa maafisa wasaidizi wa uchaguzi katika ngazi za kata na vijiji. Katika mafunzo hayo, Bieda amewakumbusha wasimamizi hao kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu zote za uchaguzi, huku akisisitiza umuhimu wa kutunza siri zote zinazohusu mchakato mzima wa uchaguzi.

Aidha, Afisa Uchaguzi wa Halmashauri hiyo, Bi. Grace Haule, ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kujiandikisha ili kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa. “Kila mwananchi mwenye sifa ya kushiriki uchaguzi huu asisite kutumia haki yake ya kikatiba ya kupiga kura,” alisema Haule.

Naye Hakimu Mkazi Joseph Raphael Luoga amewakumbusha maafisa hao kuheshimu viapo vyao kwa uaminifu na kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni, na taratibu zote za uchaguzi katika utendaji wao.

Miongoni mwa wasimamizi wasaidizi waliopata mafunzo, Bi. Angela Manzi, ameushukuru uongozi wa halmashauri kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa yamewaandaa kwa uadilifu na umakini katika kutekeleza majukumu yao ya kusimamia uchaguzi.

Kwa kumalizia, Bi. Bieda amesema kuwa mafunzo haya ni sehemu muhimu ya maandalizi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024. Wananchi zaidi ya 78,000 wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wanatarajiwa kujiandikisha na kupata fursa ya kuwachagua viongozi wa vijiji na vitongoji.






Related Posts