MATAMPI: Huyu Camara amekuja kuongeza vita

Msimu wa 2023/24, aliwaacha mbali Djigui Diarra ‘Yanga’ na Mohamed Mustapha ‘Azam FC’ akitwaa tuzo ya kipa bora si mwingine ni Ley Matampi ambaye amesisitiza kuwa na msimu huu pia anaitaka.

Kipa huyo tayari ameruhusu nyavu zake kutikiswa kwenye kila mchezo kati ya mechi sita walizocheza lakini amesema hilo halimpi taabu kwani kwake ni bora kucheka mwisho na sio mwanzo.

Mwananchi limepata nafasi ya kuzungumza na kipa huyo bora wa msimu ulioisha akifunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutetea tuzo yake na kumtaja kipa namba moja wa Simba, Moussa Camara kuwa ujio wake umeongeza vita mpya na hayupo tayari kuachia nafasi hiyo.

Matampi ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa kipa bora msimu uliopita, akiwaacha Diarra na Mustapha kutokana na kuongoza kwa ubora ndani ya kikosi cha Coastal Union iliyomaliza nafasi ya nne msimu ulioisha, amesema  ongezeko la Camara kwenye ligi ni vita mpya.

“Ukiondoa ujio wa Camara, uwepo wa Diarra na Mustapha kuna makipa wengine wengi wanafanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara, ninachotakiwa kukifanya ni kuongeza juhudi ili kuendeleza ubora wangu na kujiweka kwenye ushindani,” anasema na kuongeza;

“Natambua ubora wa kila mmoja na ujio wa Camara ambaye amejiunga na Simba unaendelea kuongeza chachu ya ushindani hasa kwenye eneo la kipa, namfahamu Diarra, Mustapha kwa sababu tulikuwa wote msimu ulioisha Camara ni kipa mzuri na uwepo wake unaongeza vita ili tupambane zaidi.’’

Dirisha kubwa la usajili mengi yalizungumzwa kuhusiana na Matampi kutua Simba lakini haikuwa hivyo kipa huyo amefunguka sababu kuwa ni uongozi.

“Ni kweli kulikuwa na mazungumzo kati yangu na Simba kwa ajili ya kuitumikia msimu huu lakini mambo yalienda tofauti kutokana na viongozi wa Coastal Union kufanya mazungumzo na mimi ili kutoa uzoefu kwa vijana waliopo.

“Viongozi walikaa chini na mimi wakiniomba niendelee kusalia ndani ya Coastal Union ili niweze kuwafundisha vijana waliopo kutokana na uzoefu nilionao.”

Matampi anasema bado kuna muda kama ikitokea nafasi nyingine atafanya hivyo ila kwa sasa ni mchezaji wa Coastal Union haoni sababu ya kuzungumza masuala yaliyopita.

Wakati wadau wengi wakiikatia tamaa Coastal Union kutokana na matokeo mabaya ya mechi sita za mwanzo wakipoteza nne sare moja na kushinda moja, Matampi anasema ni mapema sana kuwatoa kwenye reli.

“Sishtushwi japo sio mipango yetu lakini ukweli ni kwamba hata msimu uliopita nakumbuka mechi tano tulikuwa na pointi mbili hivyo kilichopo ni kuendeleza mapambano tu ili kuweza kufikia malengo,” anasema na kuongeza;

“Matokeo yaliyopo sasa yanatuumiza na hatufurahishwi na kinachotokea lakini tunaamini kila kitu kinawezekana tukiwekeza nguvu kwa kuongeza juhudi za mapambano uwanjani.”

Licha ya kuachwa mbali na baadhi ya makipa ambao wanaongoza kwa kuzisaidia timu zao kutoruhusu mabao kwenye mechi walizocheza wakiongozwa na Mussa Mbisa (Tanzania Prisons) ambaye ameiongoza timu yake kwenye mechi nne bila kufungwa, Camara mechi tatu kipa huyo anasema.

“Ni kweli kuna makipa tayari wameziongoza timu zao bila ya kuruhusu mabao hilo kwangu wala halinipi shida kwani naamini kwenye mwisho kuliko mwanzo, nina uwezo wa kutetea tuzo yangu kwani kuna mechi nyingi mbele.

“Nawapongeza makipa ambao tayari wameweka rekodi ya kutofungwa hadi sasa, nawaambia kuwa mimi ni Matampi na nitabaki kuitwa hivyo sishindani na mtu nashindana na mimi mwenyewe kwa kuweka malengo ambayo ni kujiweka kwenye nafasi ile ile ya msimu uliopita.”

Matampi msimu huu ni wa pili kwake akiitumikia Coastal Union baada ya msimu ulioisha kuisaidia kumaliza nafasi ya nne na kushiriki michuano ya kimataifa amefunguka kuwa msimu ujao pia wanaitaka nafasi hiyo na hakuna kinachoshindikana.

“Ni mapema sana kuiondoa timu yetu kwenye nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa mimi bado naamini tuna nafasi hiyo na tunaweza endapo uongozi utawekeza nguvu,” anasema na kuongeza;

“Uongozi ukiwekeza juhudi na jitihada zao zote kwa kuijenga timu vyema kisaikolojia na kutengeneza mazingira mazuri kuanzia juu hadi kwetu wachezaji hakuna kinachoshindikana na bado tuna michezo mingi ambayo inaweza kuturudisha kwenye ushindani.”

SABABU KUKOSA MECHI ZA CAF

Awali ilikuwa inaelezwa kipa huyo alisaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Coastal Union na hatakuwa sehemu ya kikosi hicho msimu huu lakini mambo yameenda tofauti anaendelea kuitumikia timu hiyo.

“Ni kweli kulikuwa na mgogoro wa kimkataba kutokana na kupishana na viongozi kwenye makubaliano lakini sasa nipo ndani ya timu mara baada ya kukaa nao na kumalizana kama ambavyo mimi nilikuwa nataka sioni sababu ya kuzungumza mambo yaliyopita.

“Sababu ya mimi kuchelewa kujiunga na timu na kukosa baadhi ya michezo ya kimataifa ni kutokana na kutomalizana na viongozi na nimerejea baada ya makubaliano yangu na klabu kwenda sawa sasa acha kazi iendelee na kila mmoja ataona ubora wangu uwanjani.” anamalizia.

Related Posts