Msikiti uliojengwa 1826 kuvunjwa kupisha ujenzi wa barabara Mbeya

Mbeya. “Historia inaenda kufutika”. Hiyo ni kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga, akielezea kuvunjwa kwa msikiti mkongwe uliopo mji mdogo wa Mbalizi wilayani Mbeya mkoani hapa. kupisha ujenzi wa barabara ya Mbalizi – Makongolosi.

Msikiti huo ambao umedumu kwa miaka 198 tangu ulipojengwa mwaka 1826, umekuwa wa kihistoria na kivutio ambapo mbali na waumini kuutumia kwa ibada, lakini umekuwa kumbukumbu na kuenzi kazi na mchango wa wazee wa zamani.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kwenye sherehe za Maulidi zilizofanyika kimkoa wilayani humo usiku wa Septemba 29, 2024, Batenga amesema pamoja na msikiti huo kuwa na historia kubwa mkoani humo, lakini unakwenda kuvunjwa kupisha ujenzi wa barabara.

Amesema Serikali inahitaji maendeleo na kusogeza huduma kwa wananchi, hivyo barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami na msikiti huo utabomolewa kupisha ujenzi huo.

 Amewapongeza viongozi wa dini mkoani humo kwa kuanza ujenzi wa msikiti mpya.

“Wazee waliotangulia walifanya makubwa na niwashukuru viongozi kwa kuanzisha ujenzi wa msikiti mwingine, historia inaenda kuvunjwa kupisha ujenzi wa barabara ya lami hadi Makongolosi na haya ndiyo maendeleo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Naambiwa msikiti huu ulikuwa wa matete, baadaye waliofuata wakaukarabati kuuweka katika hali hii na leo sisi tunajenga mwingine na huenda watakaofuta watajenga mwingine. Niwapongeze viongozi wa dini kwa kujenga huu mpya unaogharimu zaidi ya Sh42 milioni ili kuendelea kuwaenzi wazee wetu,” amesema Batenga.

Alipoulizwa kuhusu kuvunjwa kwa msikiti huo, Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata) Mkoa wa Mbeya, Sheikh Mtawa Kapalata amesema walishaomba muda mrefu usivunjwe lakini ikashindikana, hivyo wanakubaliana na kitakachofanyika kwani hawawezi kuzuia maendeleo.

“Ndiyo maana tumeanza kujenga msikiti mwingine mpya kwa kuacha eneo hilo ambalo linapitiwa na barabara, historia itabaki kwenye makaratasi kwamba ulikuwapo msikiti mkongwe,” amesema Sheikh Kapalata.

Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Mbeya ambao ndiyo wanaojenga barabara hiyo, Mhandisi Matari Masige amesema iwapo msikiti huo utakuwa ndani ya barabara hauwezi kuachwa, lazima utabomolewa.

“Siwezi kuliongelea zaidi kwa kuwa siufahamu (msikiti), lakini kama utakuwa kwenye hifadhi ya barabara hauwezi kuachwa, hata ungekuwa na miaka 400, lazima utapitiwa tu,” amesema meneja huyo alipoulizwa kama kuna uwezekano wa kuuacha.

Ramadhan Lehani (92) ambaye alisoma elimu ya dini (madrasa) katika msikiti huo, miaka ya 1938 hadi 1940, amesema amepokea kwa masikitiko taarifa ya kuvunjwa kwa msikiti huo akieleza kuwa angefurahi iwapo sheria itaruhusu eneo hilo libaki kama ukumbusho.

Amesema msikiti huo ulianza kutumika ukiwa wa nyasi ambapo miaka hiyo, yeye akiwamo, walibadilisha mwonekano kwa kuweka tofali za kuchoma badala ya mbichi zilizokuwepo, hivyo kama utavunjwa utaondoa historia ya watangulizi.

“Nimesoma hapo madrasa miaka ya 1938 hadi 1940 na mwalimu wetu aliitwa Sheikh Hamza Mwinzagu, enzi hizo ukiwa na nyasi na tofali mbichi ambapo baadaye tukaubadilisha tukaweka tofali za kuchoma kisha bati, binafsi sijashirikishwa katika kuvunjwa kwake badala yake nasikia hizo taarifa tu.

“Nashauri kama sheria zitaruhusu msikiti huo uachwe, ubaki kama makumbusho na historia, zamani walikata eneo la barabara upande wa juu, sasa sijajua itakuaje kwa sasa,” amesema Lehani.

Ameongeza kuwa hakukuwepo matumizi mengine zaidi ya waumini kufanya ibada na shughuli nyingine za dini, huku akibainisha kuwa hadi sasa ni kivutio na historia ya zamani.

Mmoja wa majirani wa msikiti huo ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amesema kutokana na msikiti huo kubeba historia ya eneo hilo, ungeachwa kwa kufanywa kivutio na sehemu ya kuenzi kazi za waliotangulia (makumbusho).

“Kila sehemu na kivutio chake, ninashauri bora ungeachwa ili ubaki historia kwa vizazi vijavyo, isitoshe hii ni nyumba ya ibada, siyo eneo la mtu kibiashara. Tungeutumia kama makumbusho na watu kuja kujifunza,” amesema.

Related Posts