NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA FEDHA, BW. MWANDUMBYA AFUNGUA MKUTANO WA IIA NA VIONGOZI TAASISI ZA UMMA NA BINAFSI, ARUSHA

Mkutano kati ya Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA) na viongozi wa taasisi za umma na sekta binafsi ukiendelea.


Rais wa Wakaguzi wa Ndani Tanzania, Dk. Zelia Njeza akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hafla ya ufunguzi wa Mkutano kati ya Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA) na viongozi wa taasisi za umma na sekta binafsi.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya (kulia) akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua Mkutano kati ya Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA) na viongozi wa taasisi za umma na sekta binafsi, kushoto ni Rais wa Wakaguzi wa Ndani Tanzania, Dk. Zelia Njeza akifuatilia.

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya leo amefungua Mkutano kati ya Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA) na viongozi wa taasisi za umma na wa sekta binafsi uliolenga kujadili na kuboresha masuala mbalimbali ya kiutawala, pamoja na kubadilishana uzoefu ili kuziwezesha taasisi zao kufanya vizuri zaidi kiufanisi.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya kufungua mkutano huo, Bw. Mwandumbya ameipongeza taasisi ya IIA kwa kuwakutanisha viongozi wa taasisi hizo na kujengeana uwezo kwa malengo ya boresha zaidi ufanisi katika taasisi zao, hii ikiwa ni mara ya 11 viongozi hao wanakutanishwa kujadili masuala mbalimbali ya uboreshaji utendaji na ufanisi kwa taasisi za umma na binafsi.

Alisema kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuwajengea uwezo wakaguzi wetu wa ndani kwani uchumi wetu unapitia kwenye mabadiliko makubwa, ambayo yana fursa kubwa na bila kujali changamoto zilizopo ndani yake. Hivyo kujengeana uwezo kwenye mazingira haya ni jambo la msingi.

Mwandumbya amesema kuna haja ya kuangalia maeneo mbalimbali katika uchumi wa nchi yetu na dunia kwea ujumla na kujiandaa kukabiliana na changamoto za kiuchumi zilizopo ndani ya nchi kuelekea katika mabadiliko ya kidigitali.

Ameongeza kuwa, Serikali inataka kuona wakaguzi wanakuwa na msimamo mzuri, unaoweza kuhakikisha mabadiliko yanafanywa ili kuboresha utendaji kazi wa taasisi mbalimbali kuchochea maendeleo.

Aidha ameongeza kuwa, pamoja na mambo mengine bado suala la uadilifu kwa watendaji na vyombo vyao ni suala la msingi, ambalo limekuwa likisisitizwa kwa wakaguzi wote. “Taasisi inapaswa kuwekeza kwenye uadilifu kwani suala hilo ndio nguzo kuu ya kuweza kutoa maoni yao ili kuboresha matokeo ya taasisi wanazoziongoza,” alisisitiza kiongozi huyo.

“Kwenye suala la usimamizi wa rasilimali za nchi ni muhimu sana kuwekeza kwenye uadilifu “amesisitiza.

Kwa upande wake Rais wa Wakaguzi wa Ndani Tanzania, Dk. Zelia Njeza amesema taasisi hiyo itakuwepo mkoani Arusha kwa ajili ya Mkutano mkubwa wa viongozi, taasisi mbalimbali utakao jadili mambo yanayojitokeza kwenye mazingira ambayo wanafanyia kazi na kushirikishana namna ya kuyaboresha zaidi kwa lengo la kuleta ufanisi. 

Amesema, kutokana na mabadiliko mbalimbali ambayo yanajitokeza katika mazingira wanayofanyia kazi nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla, na hata dunia nzima kwa ujumla sisi kama viongozi ni lazima kutathmini kazi zetu.

“Ni vizuri tuweze kuwa na taarifa na kujifunza mabadiliko haya ambayo yanajitokeza na tutajikita kujadili mambo yetu wenyewe na ipo haja ya wahusika kubadilika katika kuendana na kasi ya mabadiliko ambayo yanajitokeza kwenye upande wa teknolojia, hali ya hewa na mambo mbalimbali,” amesema Dk. Njeza.

Amesema ifikapo Oktoba 2, 2024 IIA pamoja na wadau wake watakuwa na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wakaguzi wa ndani, ambapo Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi ndiye anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Related Posts