Neema, Vicky wafichua kinachowabeba | Mwanaspoti

Mchezaji wa timu ya taifa ya gofu wanawake, Neema Olomi ameiita michuano ya Lina PG Tour ni ‘tanua mbavu’ kwa wacheza gofu wanawake kwani inawalazimisha kutumia ujuzi na maarifa zaidi ili kufanya vizuri.

Olomi na mchezaji mwenzake Vicky Elias wamesema mjini Moshi jana kuwa ugumu huu ndiyo siri ya wao kufanya vizuri katika mashindano makubwa nje ya nchi.

“Viwanja vya nyumbani ni vigumu mno ukilinganisha na vile vya nchini Kenya, Uganda na Zambia. Ili kushinda michuano ya Lina PG Tour jasho la damu lazima likutoke,” alisema Olomi baada ya kumaliza mashimo 54 ya mchezo siku ya Jumamosi.

“Nimefanya kazi kubwa sana kuipambania nafasi hii kwa sababu katika mashindano haya kuna wachezaji wengi mahiri, wengi wao wakiwa na viwango cha chini ya handicap 5. Inabidi kufanya zaidi ya jitihada ili kufuzu hatua za mchujo ili nipate nafasi ya kucheza mashimo yote 72,” alisema.

Neema na mwezake Elias ambaye alimaliza katika nafsi ya tisa nyuma ya wachezaji wanane wa kiume, wamesema mashindano ya ndani ni mtihani mzuri kwao.  

“Katika mashindano tunayocheza mara kwa mara nchini Kenya au Uganda mara nyingi tunapiga kuanzia +2 had +6, na tunashinda, lakini kwa Tanzania ni nadra kupiga chini ya +10,” alisema Olomi.

Kufutia hali hii wachezaji hawa wameona ugumu wa mashindano yanayofanyika nchini yakiwemo ya Lina PG Tour kama ni fimbo inayowaamsha wao kufanya vizuri nje ya nchi.

Kabla ya kucheza mashindano ya Uganda Open ambayo ni michuano yao ya mwisho nje ya nchi, Olomi alimaliza wa pili katika mashindano ya viwanja vitano katika mwambao wa Kenya wakati Vicky Elias akimaza katika nafasi ya tatu.

Nchini Uganda, Watanzania walitawala tena John Walker Uganda Open ambako Madina Iddi alishika nafasi ya kwanza na kufuatiwa na Hawa Wanyeche katika nafasi ya pili wakati Olomi na Vicky wakichukua nafasi za tatu na tano.

“Naamini baada ya mazoezi ya kina kupitia mashidano haya, Tanzania itawakilishwa vyema katika mashindano ya gofu ya ubingwa wa Afrika nzima nchini Morocco mwezi Novemba mwaka huu,” alisema Olomi.

Related Posts