Rais Samia amteua Karume kuongoza Misheni ya SADC uchaguzi wa Msumbiji

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume amewasili jijini Maputo nchini Msumbiji jana Jumapili, Septemba 29, 2024 kuongoza Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC SEOM) katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaotarajia kufanyika Oktoba 9, 2024.

Karume ameteuliwa kuongoza misheni hiyo na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (Organ) kuanzia Agosti, 2024 hadi Agosti 2025.

Akiwa nchini Msumbiji, Karume atazindua misheni hiyo Oktoba 3, 2024.  Aidha, kwa kushirikiana na wajumbe wa Troika (Tanzania, Zambia na Malawi) anatarajia kukutana  na wadau mbalimbali wa uchaguzi, ikiwemo  Tume ya Uchaguzi ya Msumbiji (CNE),  mabalozi wa nchi za SADC  waliopo Msumbiji, vyama vya siasa,  asasi za kiraia, taasisi za kidini na vyombo vya habari.

Pia Oktoba 11, 2024, Mkuu wa Misheni, Karume anatarajiwa kutoa taarifa ya awali ya Misheni ya SADC baada ya uchaguzi nchini Msumbiji kukamilika.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts